Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk .Stargomena Tax amesema katika kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru, na usalama wa nchi, Wizara hiyo kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limechangia kujenga uchumi imara ambapo wananchi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu.
Pia amesema kuwa Wizara inatoa shukrani za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kutoa uzito wa kipekee kwa wizara na taasisi zake, hususan kuliboresha na kuliimarisha jeshi, kuimarisha viwanda vya jeshi, na kuimarisha diplomasia ya ulinzi
Hayo yamesemwa jijini Dodoma leo Aprili 3,2024 na Waziri Tax wakati akizungumzia kazi zilizofanywa pamoja na mafanikio ya wizara hiyo kupitia sekta ya ulinzi katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar amesema kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mipango madhubuti katika ulinzi wa nchi, vinatoa fursa kwa wananchi kujikita katika ujenzi wa Taifa lao.
Ameeleza kuwa suala la amani na utulivu vilivyopo nchini ni moja ya mafanikio ya kazi iliyofanywa na Wizara hiyo kupitia sekta ya ulinzi kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano ambapo kunaifanya nchi kuwa shwari tangu wakati wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi sasa.
"Serikali kupitia Wizara imeendelea kutekeleza, na kuliimarisha Jeshi kwa kulipatia zana na vifaa bora na vya kisasa, rasilimali watu, na nyenzo za kufanyia mazoezi ili kuwa imara wakati wote," ameeleza.
Waziri Tax ameongeza kuwa ili kuliimarisha Jeshi, Serikali kupitia Wizara imeendelea kuboresha maslahi kwa Wanajeshi na Watumishi wa Umma kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu, kwa kuwapatia makazi bora kwa kuwajengea nyumba, pamoja na stahili mbalimbali, kupandisha vyeo kulingana na sifa, vigezo na taratibu’’, alisema Waziri huyo.
Ametaja baadhi ya mafanikio ya wizara hiyo amesema ni pamoja na kutungwa kwa Sheria ya JKT Na. 16 ya mwaka 1964 (The National Service Act No. 16 of 1964) ambayo iliwezesha kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Amefafanua kuwa hadi sasa Serikali imejenga nyumba za makazi katika kambi mbalimbali za Jeshi kwenye Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Mwanza, Pemba, Pwani, Rukwa, Tabora, na Tanga. Aidha, ujenzi wa nyumba hizo, kwa kiasi kikubwa umepunguza uhaba wa nyumba pamoja na changamoto zitokanazo na wanajeshi kuishi uraiani.
Aidha Waziri Tax ametaja mchango mwingine mkubwa wa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania katika miaka 60 ya Muungano, ni ulinzi madhubuti wa mipaka yetu, uhuru, na katiba kwani Nchi imeendelea kuwa imara na yenye amani katika awamu zote.
Waziri Tax amesema mafanikio mengine ni ushiriki wa Wizara kupitia Taasisi zake, hususan JWTZ katika kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pale yanapotokea.
Ameongeza kuwa katika kutekeleza jukumu hilo, JWTZ imeendelea kushiriki kikamilifu katika kutoa misaada ya uokoaji na ile ya kibinadamu kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.A: JT
0 Comments