MAJAJI WA RUFANI WAONGEZEKA KIPINDI CHA RAIS DK. SAMIA


Na Asha Mwakyonde, Dodoma

IDADI ya Majaji wa Rufani imeongezeka na kufikia 35 ikiwa ni zaidi asilimia 100 katika kipindi cha uongozi  wa Dk. Samia Suluhu Hassan tangu alipoiingia madarakani Machi 2021 ambapo kulikuwa na Majaji wa Rufani 16 hadi kufikia  Septemba 3, 2023.

Hayo yamesemwa leo Aprili 5, 2024 Jijini Dodoma  na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Elisante Ole gabriel wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kuelekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na zanzibar na ongezeko la majaji mahakama ya Rufani Tanzania. 

Amesema ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufani limeenda sambamba na uanzishwaji wa Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani nchini.

Prof. Elisante amesema kuwa Wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kumekuwepo na ongezeko la Majaji wa Rufani.

"Mahakama ya Rufani inapata mamlaka yake kutoka katika Katiba na Sheria zilizotungwa na Bunge ambapo Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, 1979 ilitoa mamlaka kwa Mahakama ya Rufani za Mahakama Kuu za Tanzania na Zanzibar," amesema.

Kwa mujibu wa Gabriel katika kusikiliza rufaa, Majaji watatu wanaunda Mahakama Kamili na uamuzi wa Mahakama ni wa walio wengi. Katika matukio mengine, Majaji watano, au Majaji saba, wanaweza kuunda Mahakama kutegemea na shauri husika linalosikilizwa,Jaji mmoja anaweza kukaa katika chumba chake kusikiliza maombi ambayo yanastahili kuamuriwa. 

Amengeza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) na 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chombo chenye mamlaka na kauli ya mwisho katika  kutekeleza utoaji haki  ni  Mahakama ya Tanzania. Mahakama ya Tanzania inajumuisha Mahakama ya Rufani ambayo utoa huduma kwa pande zote za Muungano.

"Mahakama ya Rufani ndiyo Mahakama ya juu kuliko zote nchini Tanzania ambayo ilianzishwa chini ya Ibara ya 117 (1) ya Katiba ya Tanzania, 1977. Jaji Mkuu ambaye huteuliwa na Rais ndiye Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Rufani," ameeleza.

Amesema katika shughuli za kila siku za Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu husaidiwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani, kama Mkuu wa Masjala ya Mahakama, Naibu Msajili Mwandamizi na Naibu Wasajili wa Mahakama hiyo, Msajili wa Mahakama ya Rufani  husimamia utendaji wa kazi za Mahakama, kuratibu na kuwasiliana na Jaji Mkuu kuhusu masuala yanayohusu shughuli za kila siku za Mahakama.

Kwa mujibu wa Muundo mpya wa Mahakama, usimamizi wa kila siku wa shughuli za kiutawala na uendeshaji wa Mahakama kwa Mahakama ya rufani husimamiwa na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani.

Akizungumzia Muungano amesema watumishi wengi wa mahakama wanatokea katika Muungano  na kwamba wanaamini haki ya Muungano ni utoaji wa haki.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU