Na. Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma
Serikali itaendelea kufuatilia malikale zote ambazo zilichukuliwa kabla na baada ya uhuru kwa ajili ya kuzitambua na kufanya utaratibu wa kuzirudisha nchini.
Haya yamebainika leo Mei 3, 2024 wakati Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) akijibu swali la Mhe. Condester Michael Sichalwe ambaye alitakujua Kimondo kilichoanguka katika kijiji cha Ivuna kitarejeshwa lini nchini ili kutumike kama Kivutio cha Utalii katika mkoa wa Songwe.
Aidha, Mhe. Kitandula amesema kuwa serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya kuishauri namna bora ya kurudisha au kunufaika na malikale zilizo nje ya Nchi.
Vilevile Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Kimondo cha Ivuna kinahifadhiwa kwenye Makumbusho ya Historia Asili (Natural History Museum) iliyopo katika Mji wa London Nchini Uingereza.
“Kimondo kilichoanguka Kijiji cha Ivuna, Mkoa wa Songwe Mwaka 1938 kikiwa na ujazo wa tani 0.0077 sawa na asilimia 0.0044 ya kimondo cha Mbozi kilichopo katika Kijiji cha Isele Mkoani Songwe chenye tani 16” Alisema Mhe. Kitandula
Ili kuvutia watalii kwenye eneo la Ivuna kilipoangukia kimondo hicho, wizara ya Maliasili na Utalii itafungamanisha eneo hilo na tamasha la vimondo ambalo hufanyika mwezi Juni kila mwaka, tukio ambalo hutumika vilevile kutangaza tamaduni, mila na desturi za watu wa Songwe.
0 Comments