WAZIRI BASHE: ASA ILIPANGA KUZALISHA TANI 5,000 ZA MBEGU BORA,TANI 3,593.4 ZIMEPATIKANA


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA),ilipanga kuzalisha na kusambaza tani 5,000 za mbegu bora za alizeti na ngano kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku ambapo hadi Aprili, 2024 jumla ya tani 3,593.4 zimepatikana ambapo tani 1,619 ni za ngano na tani 1,974.4 ni za alizeti.

Akiwasilisha hotuba yake ya makadirio,mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, leo Mei 2,2024 Jijini Dodoma karibuni Hussein Bashe amesema tani 1,015 kati ya tani 1,619 za ngano zimesambazwa kwa mpango wa ruzuku katika mikoa ya Njombe, Rukwa, Mbeya, Manyara, Arusha na Kilimanjaro. 

Waziri huyo ameeleza kuwa ,tani 725 kati ya tani 1,974.4 za mbegu za alizeti zimesambazwa kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku katika mikoa ya Singida, Dodoma, Manyara, Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Geita.

"Wizara kupitia ASA,Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), na Bodi za mazao ilipanga kuzalisha miche 37,500,000 ya mazao mbalimbali," ameeleza Waziri Bashe.

Ameongeza kuwa hadi Aprili, 2024, jumla ya miche 29,261,780 ya mazao ya kahawa (21,899,560), chai (3,048,000), mkonge (2,413,277), korosho (239,762), chikichi (307,588), parachichi (647,724), zabibu (338,101), minazi (75,000), viazi (278,155), miwa (4,543) na migomba (10,070) imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika mikoa ya Songwe, Kagera, Kilimanjaro, Njombe, Iringa, Tanga, Morogoro, Kigoma, Tabora na Mbeya.

Amefafanua kuwa pingili za muhugo 4,438,170 zimezalishwa na kusambazwa kwa wakulima 267,145 katika mikoa ya Mara, Morogoro, Pwani, Mwanza, Geita, Kigoma, Katavi, Tabora, Singida, Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Waziri Bashe amesema katika mwaka 2023/2024 wizara hiyo ilipanga kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora nchini kwa kuendelea kuiwezesha ASA kujenga na kukamilisha miundombinu ya umwagiliaji yenye jumla ya hekta 3,304.8 ifikapo mwaka 2025 katika mashamba yote ya mbegu ya ASA ya Kilimi hekta 300, Msimba hekta 400, Bugaga hekta 100, Mbozi hekta 400, Luhafwe hekta 400, Dabaga hekta 300, Namtumbo hekta 500, Arusha hekta 100, Kilangali hekta 300, Mazizi hekta 4.8, Msungura hekta 100 na Mwele hekta 400.

"Wizara ilipanga kuiwezesha ASA kununua vitendea kazi vikiwemo matrekta kumi na zana zake ninaomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa ASA imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yenye ukubwa wa hekta 805.5 iliyopangwa katika mwaka 2022/2023 na hekta 795 zilizopangwa katika mwaka 2023/2024," amesema.

Amesema hadi Aprili, 2024 utekelezaji umefikia katika hatua zaujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa hekta 220 kati ya 400 katika shamba la Kilimi umekamilika na ukamilishaji wa eneo la hekta 180 katika shamba hilo unaendelea.

Waziri huyo ameeleza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la Arusha hekta 200 umefikia asilimia 55,ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika Shamba la Msimba hekta 200 umefikia asilimia 45 pamoja na ujenzi wa bwawa lenye ujazo wa lita milioni 45 katika shamba la mbegu Arusha umekamilika.

Waziri Bashe amefafanua kuwa ujenzi wa bwawa lenye ujazo wa lita milioni 45 katika shamba la Msimba umefikia asilimia 70 na uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji kwa njia ya matone katika shamba la Tengeru lenye ukubwa wa hekta 5.5 umekamilika.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la Namtumbo hekta 300 utekelezaji upo katika hatua ya kumpata mshauri elekezi na kwamba Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya Mbozi hekta 100, Arusha hekta 100 na Msimba hekta 100 utekelezaji upo katika hatua za kusaini mkataba.

 "ASA imeendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya mbegu yenye ukubwa wa hekta 3,000 mashamba haya ni Mwele hekta 500, Namtumbo hekta 900, Kilimi hekta 200, Msungura hekta 100, Mbozi hekta 500 na Msimba hekta 800," ameeleza.

Ameeleza kuwa hadi Aprili,2024 utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu upo katika hatua ya tathmini ya kumpata mshauri elekezi na hiyo Wizara ilipanga kuiwezesha ASA kujenga ghala katika mashamba ya Arusha, Mbozi, Namtumbo, Msungura na Kilangali; kununua na kufunga mitambo miwili ya kuchakata mbegu katika mashamba ya mbegu ya Mbozi na Namtumbo; na kulipa fidia ya mashamba mapya ya mbegu ya Tanganyika (Luhafwe), Namtumbo na Chalinze (Msungura na Mazizi).

Waziri huyo amesema hadi kufikia Aprili, 2024 taratibu za manunuzi ya wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa ghala la Arusha zimefikia hatua ya kusaini mkataba na mshauri elekezi na kwamba, taratibu za ununuzi wa mitambo miwili (2) ya kuchakata mbegu katika mashamba ya mbegu ya Mbozi na Namtumbo zipo katika hatua ya tathmini.

 "Ili kuzuia uvamizi wa mashamba ya mbegu, ASA imekamilisha ujenzi wa uzio katika mashamba ya Msimba – Kilosa hekta 2,600 na Kilimi – Nzega hekta 1,102, na ujenzi wa uzio katika shamba la Arusha hekta 600 utekelezaji upo katika hatua ya tathmini ya kumpata mkandarasi," ameeleza.

Ameongeza kuwa ASA imenunua magari matatu, pikipiki nne mashine za kupandia mpunga mbili na matrekta mapya tisa na zana zake kwa ajili ya kurahisisha shughuli za uzalishaji katika mashamba ya mbegu. 

Kwa mujibu wa Waziri Bashe Wizara kupitia ASA ilipanga kuendelea kufungua maeneo mapya katika mashamba ya Mwele hekta 300, Luhafwe hekta 400, Msimba hekta 300, Kilimi hekta 200, Namtumbo hekta 200na Mbozi hekta 200.

Amesema hadi kufikia Aprili 2024 jumla ya hekta 1,619 sawa na asilimia 101.2 ya lengo zimefunguliwa katika mashamba ya mbegu ya Kilimi hekta 260, Namtumbo hekta 389, Msimba hekta 540, Dabaga hekta 100 na Mwele hekta 330.

 Waziri Bashe amesema eneo hilo litaongeza uzalishaji wa mbegu wa takribani tani 3,000 kwa kuipatia sekta binafsi na kwamba utumiaji wa eneo hilo unaongeza ulinzi dhidi ya uvamizi wa mashamba.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI