Na Asha Mwakyonde,Dodoma
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi. Abdallah Ulega anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kesho katika maadhimisho ya siku maluum ya mchango wa punda ulimwenguni ambayo imeandaliwa na mashirika yasio ya kiserikali Shirika la Inades Formation Tanzania (IFTz), na Shirika la Ustawi wa wanyama( ASPA) lenye makao makuu katika jiji la Arusha.
Pia Wafanyabiashara wa maduka ya dawa za mifugo wametakiwa kuorodhesha dawa za mnyama punda pindi wanapotaka kuagiza dawa hizo kama ilivyo kwa mifugo mingine na kuwasiliana Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),ili waweze kupata kipali cha kuagiza.
Akizungumza leo Mei 16,2024 jijini Dodoma Mkurugenzi wa shirika la ASPA Livingstone masija amesema katika sera na Sheria ya Tanzania mnyama punda hajawekwa katika kundi la kuchinjwa na kuliwa hivyo sio mnyama wa kutoa nyama katika jamii yetu.
Mashija amesema mnyama huyo amesahulika katika jamii ya kitanzania hivyo kwa maadhimisho hayo ataanza kupewa kipaumbele, kulindwa na ikiwezekana atungiwe Sheria asije akatoweka katika jamii ya kitanzania.
"Tukizunguka maduka mbalimbali katika maduka ya mifugo huwezi kupata dawa ya minyoo,vidonda, ya kutuliza maumivu ya punda utaambiwa haipo," ameeleza.
Masija ameeleza kuwa nchi za jirani wameshaanza kwenda mbali kwa kuweka dawa ya mnyama punda hivyo Tanzania nayo iitahidi kuweka dawa hizo huku akisema soko lipo kwa Wafanyabiashara wa dawa za mnyama punda.
"Tupo hapa kwa ajili ya kuadhimisha siku maluum ya mchango wa punda dunania na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri wa mifugo na Uvuvi Ulega, kwa Tanzania tumeamua kukutana na wadau kwa muda wa siku mbili Mei 16 na 17," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa IFTz, Mbarwa Kivuvyo amesema kuwa wao kama shirika wamekuwa wakishiriki katika sekta ya kilimo kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wadogo wa mazao na wafugaji wa mifugo ya aina mbalimbali.
Kivuyo ameeleza kuwa kuanzia mwaka 2019 walikuwa na mradi ambao unashughulika na ustawi wa punda kwa ajili kuboresha maisha ya jamii maeneo ya vijijini lengo kuu ni kupata nafasi ya kumuendeleza mnyama huyo ili aweze kutoa huduma kwa jamii ya wakulima hasa wanawake na watoto.
Amesema kuwa katika Mkoa wa Dodoma wamefika Wilaya zote na kwamba lengo lao ni kuhakikisha mnyama punda anaheshimika.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Mei 8, kila mwaka ni maadhimisho ya punda ulimwenguni ambao wao wamechagua tarehe tofauti ambapo walianza tangu ya Mei 13, mwaka huu kwa kwenda bungeni kwenye maonesho yaliyokuwa yameandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ndio ilikuwa ikiwasilishwa bajeti ya Wizara hiyo ili kutoa elimu kwa wabunge na watu waliotembelea maonesho hayo.
Naye mfugaji wa punda kutoka Kijiji cha Makatapora Iringa DC, Sara Miteli amesema kuwa wapo katika maadhimisho hayo kujadili mnyama punda namna ya kumtunza huku akisema wengi wanaishi na mnyama huyo na hawajui thamani yake.
Amesema mnyama punda amempatia manufaa mbalimbali kwa kuwa Mkoa wa Iringa vijijini kuna shida ya maji hivyo mnyama huyo hutumika kubeba maji ambayo yanakaa muda mrefu tofauti na angeenda mwenyewe ambapo angepata ndoo moja ya maji.
"Mnyama punda anamsaada mkubwa kwangu na kwa jamii kwa ujumla , sisi ni jamii ya kimasai punda kwetu anatamani kuliko hata ng'ombe, punda anatubebea kuni na tunauza tunajipatia kipato," ameeleza.
Ameongeza kuwa kupitia mnyama punda kwa sasa wanawake wa vijijini wameweka akiba ya fedha na wanapatiwa mikopo kutoka taasisi za kifefha kutokana na kipato wanachokipata kila siku.
0 Comments