ASILIMIA 78 WATUMIAJI DAWA ZA KULEVYA NI VIJANA

Na Asha Mwakyonde Dodoma 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri mkuu,sera, bunge na uratibu Jenista Mhagama ameeleza idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini ni vijana kwa wastani wa asilimia 78 ambapo huathiri nguvu kazi ya Taifa.

Akizungumza jijini hapa leo Mei 16,2024 katika Viwanja vya bunge wakati akitoa taarifa na mafanikio ya hali ya dawa za kulevya nchini Waziri Mhagama amesema vijana hao ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Amesema bado wana safari ndefu katika kupambana na janga hilo huku akisema ni wazi kuwa bado dawa za kulevya zinaingia nchini kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika nchi zinazozalisha dawa hizo, kubadilika kwa teknolojia za uzalishaji na usafirishaji pamoja na utandawazi.

Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha huduma za tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanaimarishwa nchini, Serikali imenunu Boti yenye mwendo kasi (Speed Boat) ambayo pamoja na shughuli zingine itakuwa ikifanya doria baharini ili kufuatilia vyombo vinavyohisiwa kuingiza dawa zakulevya nchini kama vile Heroini, Methamphetamine na nyingine.

"Boti hii lilizinduliwa rasmi April,28 mwaka huu Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Uwekezaji huu mkubwa juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya na ukamataji mkubwa uliofanyika mwaka 2023, unadhihirisha dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, katika kupiga vita dawa za kulevya nchini,"amesema.

Ameeleza kuwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Tanzania (DCEA),kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikisha ukamataji wa jumla ya kilogramu 1,965,340.52 zikihusisha watuhumiwa 10,522 wanaume 9,701 na wanawake 821.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU