Na Asha Mwakyonde,DODOMA
WATUMIAJI wa huduma mbalimbali za bima wameongezeka kutoka milioni 6 kwa mujibu takwimu za mwaka 2021 ambapo kwa sasa ni zaidi ya milioni 12 sawa na asilimia 100 ya watumishi wa huduma hizo.
Akizungumza leo Juni 19 ,2024 jijini Dodoma kwenye banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Meneja Uhusiano na Mawasiliano Hadija Maulid, amesema kuwa mamlaka hiyo hadi sasa imawasajili watoa huduma mbalimbali za bima zaidi ya 1,600 huku akisema ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2021.
"TIRA tunashiriki katika maonesho haya ya wiki ya utumishi wa Umma kwa sababu tuna jukumu mkubwa ambalo linatajwa kisheria la kutoa elimu ya bima kwa wananchi," amesema.
Ameongeza kuwa wanajukumu ambalo wameelekezwa la kutoa elimu ambapo wanatumia majukwaa mbalimbali kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi pamoja na kushiriki kwenye maonesho mbalimbali.
Meneja Uhusiano huyo amefafanua kuwa mamlaka hiyo ina majukumu mengine mbalimbali yakiwamo kusajili watao huduma za bima , kuandaa kanuni na miongozo.
"Soko la bima linakua na watu wanaelewa umuhimu wa bima wanaongezeka pamoja na haya bado tunatoa rai kwa wananchi kutumia huduma mbalimbali za bima ili kujikinga na majanga yasiyo tarajiwa.
Amesema kuwa TIRA wapo pia kwa ajili ya kusimamia haki za wateja wa bima ikiwa ni jukumu lao huku akisema popote mteja wao akiwa na changamoto za madai,au yoyote hivyo mamlaka hiyo ipo kwa ajili ya kusimamia hilo kuhakikisha haki zote za msingi zinapatikana kwa mujibu wa taratibu ambazo zimewekwe kwenye miongozo yao.
Akizungumzia elimu ya bima kwa wananchi waliopo vijijini amesema ili kuhakikisha wananchi hao wanapata elimu hiyo mamlaka Ina kanda 10 ambazo zinahudumia mikoa yote nchini.
"Kanda zote zina mameneja, maafisa bima ambapo kazi yao kubwa ni kwenda kutoa elimu mbalimbali ya wakulima, wafugaji,wavuvi waendesha boda boda,hii yote ni kuhakikisha elimu inatolewa kwa kiasi kikubwa katika maeneo yote yakiwamo ya vijijini," alisema Hadija.
Kwa upande wake Meneja Utekelezaji Sheria na Kushughulikia Malalamiko kutoka TIRA, Okoka Mgavilenzi amesema bima ni kinga dhidi ya majanga huku akisema binadamu yoyote hawezi kuepuka majanga yakiwamo mafuriko.
Aidha amewataka wananchi kutumia huduma za bima ili majanga yanapojitokeza waweze kupata fidia na kwamba wao wanahakikisha haki za mlaji wa bima zinapatikana, na zinapatikana kwa kiwango kinachostahili.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amewaagiza TIRA kuendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu huduma za Bima ili wananchi wengi waweze kuifahamu na hatmaye kujiunga na Bima mbalimbali na hivyo kujikinga na maafa yanayoweza kujitokeza dhidi yao na Mali zao.
0 Comments