Na Asha Mwakyonde Dar es Salaam
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amekabidhi ngao ya ushindi wa tatu wa jumla kwa wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijijini hapa.
Pia wafanyakazi wa BRELA wametakiwa kuendeIea kuongeza tija katika utendaji wao ili ushindi huo uendane na kazi wanazozifanya.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam Julai 3,2024 na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Godfrey Nyaisa wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa ngao hiyo katika banda lao amesema hayo ni mafanikio makubwa kwao ikilinganishwa na mwaka jana ambapo walikuwa mshindi wa pili kwenye eneo la taasisi zinazofanya kazi kama za BRELA.
Ameeleza kuwa siri ya ushindi huo ni kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na morali ya wafanyakazi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii na kujituma na hivyo kuketa tija inayohitajika.
"Katika maonesho haya licha ya kuwa tupo kwenye maonesho lakini shughuli zote zinafanyika hapo na tupo hapa kuonesha tunahokifanya pamoja na kuwahudumia wananchi wanaofika bandani kwetu," amesema Mtendaji huyo.
Ameongeza kuwa wanatoa leseni za biashara,kusajili kampuni na kwamba wanashukuru kwa kuwa washindi wa tatu na kukabidhiwa ngao hiyo na Rais Dk. Samia huku akisema huo ni uthibitisho unaoonesha wametoka wapi walipo na wanakoelekea.
Nyaisa ameeleza kuwa mtu anayetaka leseni, kusajili kampuni huduma hizo atazipata kwenye maonesho na kwamba wanafanya kazi zao kupitia mifumo.
Mtendaji huyo amesema kuwa wanaowasajili wafanyabiashara, wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi huku akieleza kwamba hakuna mwekezaji anayefika nchini bila kupitia BRELA ambayo ni lango kuu la kutambua biashara zote.
0 Comments