WANANCHI WILAYANI NSIMBO WAFURAHIA UJENZI WA DARAJA LA IBINDI


📍Daraja lafungua fursa kwa wachimbaji wa madini 

Nsimbo, Katavi 

WANANCHI wa kata za Ibindi na Itenka katika Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wameeleza kufurahishwa na ukamilikaji wa Daraja la mawe la Ibindi lenye urefu wa mita 16 katika barabara ya Ibindi-Itenka 'A' lililojengwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Wakieleza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha mradi huo ambao umeunganisha Kata za Ibindi na Itenka na kuwezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ibindi, Bw. Lukwai Dotto, ameishukuru serikali kwa kujenga daraja hilo ambapo kwasasa wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati na uzalishaji wa mazao unaendelea ambapo wameahidi kuilinda miundombinu ya daraja hilo kwa nguvu zote ili liweze kudumu kwa muda mrefu.

” Tunamshukuru Rais Samia kwa mradi huu maana ilikua vigumu kwa wananchi kuvuka upande wa pili hasa kipindi cha masika, pia ilikua vigumu hata kwa wanafunzi kupita eneo hili lakini kwa sasa panapitika kwa urahisi na wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati", alisema.

Naye, Yusuph Shagungu mkazi wa kijiji cha Ibindi, ameishukuru TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limeweza kusaidia shughuli za usafiri na usafirishaji na wananchi wanazifikia huduma za kijamii kwa urahisi. 

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Japhet Bengesi alisema, daraja hilo limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 286 kwa kutumia teknolojia ya mawe ambayo ni nafuu pia imerahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa maeneo hayo ambao wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini na kilimo.

“Daraja hili ni kiungo muhimu kuelekea Manispaa ya Mpanda, pia wawekezaji wamefika eneo hili, kuna viwanda vya wachina ambavyo vimesaidia kukuza uchumi wa wananchi, pia utekelezaji huu umewezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi”, alisema.

Post a Comment

0 Comments

TANZANIA KUJIFUNZA TEKNOLOJIA YA MAGARI YA UMEME SINGAPORE - DKT. BITEKO