Dodoma
KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Seif Shekalaghe ameupongeza Uongozi wa Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kwa kazi yao ya uelimishaji jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia, faida za malezi bora kwa familia na ulinzi na usalama kwa mtoto.
Dkt. Shekalaghe amezungumza hayo Novemba 04, 2024 katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa WAWATA na Wizara jijini Dodoma.
Dkt. Shekalaghe amesema milango ya kushirikiana na WAWATA ipo wazi na kwamba wataalam wa Wizara wapo tayari kushirikiana kupitia wataalam wa Wizara ili kurahisisha utekekezaji wa programu hizo za uelimishaji.
Aidha Dkt. Shakalaghe amesema kwa sasa jamii imeelimika vya kutosha kuhusu vitendo vya ukatili kutokana na watu wengi na wa rika tofauti tofauti kuripoti matukio ya ukatili yanayotokea katika jamii.
Naye Mwenyekiti wa Chama hicho Evaline Malisa akiwasilisha taarifa ya utekekezaji wa miradi inayohusu Wanawake na Watoto ameiomba Wizara kutoa idhini kwa WAWATA kufanya kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia itakayowafikia jamii kupitia vyombo vya Habari mbalimbali na mikusanyiko ya Makundi mbalimbali ya watu ikiwemo mikusanyiko ya waumini wa Kanisa Katoliki na maeneo mengine nchini.
0 Comments