KAMATI YA BUNGE SHERIA YAPONGEZA MAENDELEO YA MATUMIZI YA NeST

Na Mwandishi wetu, Nanyamba Mtwara 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo imeipongoza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma PPRA kwa hatua ya uboreshaji wa changamoto za Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki – NeST, pamoja na kuzitaka Taasisi zote za Ununuzi Nchini kuwa tayari na kuendelea kufanya shughuli zote za Ununuzi wa Umma kwa kutumia Mfumo wa NeST.

Pongezi hizo zimetolewa leo Februari 8, 2025 na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Wilaya ya Nanyamba Mheshimiwa Abdallah Chikota walipokuwa katika Mafunzo kuhusu Mfumo wa NeST yaliyoandaliwa na kuendeshwa na PPRA katika Ukumbi wa VETA Jijini Arusha.

Chikota amesema kuwa, mategemeo ya Serikali kupitia sekta ya Ununuzi ni makubwa ndiyo maana Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta hiyo ili kupata matokeo chanya yenye tija kwa wananchi wake na taifa kwa ujumla.

“Mkurugenzi kwa niaba ya mwenyekiti na kamati yetu, sisi tunapenda kukutia moyo na kukuomba kuendelea na roho hii ya kizalendo kwa taifa katika kuisimamia Sheria hii ya Ununuzi wewe na watendaji wako, tunaamini kwa kasi hii mnayokwenda nayo changamoto zote zinazoukabili mfumo wetu pamoja na sekta ya ununuzi kwa ujumla zitaweza kuboreshwa kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa Ujumla” amesema Chikota.



Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA Dkt. Leonada Mwagike amesema PPRA itaendelea kushirikiana kwa karibu sana na wadau wote wa Ununuzi Nchini ili kuhakikisha sekta hiyo nyeti inazidi kuimarika siku hadi siku kwa lengo la kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa.

“Waheshimiwa wajumbe, tunatambua kuwa Sheria hii ni ya kwenu na sisi ni watekelezaji tu, hivyo hatutasita kuendeleza kushirikiana nanyi kwa kupokea maoni mnayoyatoa au kuleta kwenu maoni yanayotolewa na wadau wengine wa Ununuzi kwa lengo la kuboresha pale patakapoonekana kuwa na mapungufu au changamoto ya aina yoyote” amesema Dkt. Mwagike.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa PPRA Bw. Dennis Simba amefurahishwa na muitikio wa wajumbe wa kamati hiyo na kuwaomba kuendelea kuwa mabalozi wa kuhubiri ukidhi wa Sheria Na. 10 ya Ununuzi wa Umma sambamba na utayari wa taasisi za Serikali katika matumizi sahihi ya mfumo wa NeST katika Ununuzi wa Umma kwa maendeleo endelevu ya taifa. 

Aidha, amesisitiza kwa kutoa mifano ya taasisi za umma zilizofanikiwa katika matumizi ya Mfumo wa NeST katika Utoaji wa Zabuni ambapo amezitaja kuwa ni Pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ambayo imekuwa kinara kwa kutoa jumla ya zabuni 2,065, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe iliyotoa jumla ya zabuni 1,087 huku nafasi ya tatu ikishikiliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

“Waheshimiwa Wabunge takwimu hizi zinaonesha ni kwa kiasi gani Halmashauri tajwa hapo juu zinapatikana pembezoni mwa miji, kwahivyo ni wazi kuwa taasisi zinazokwepa kufanya Ununuzi ndani ya Mfumo ni kutokana na kutokuwa na utayari wa matumizi ya Mfumo na si kwa sababu za kimtandao kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.”

Hata hivyo, ameongeza kuwa Mfumo wa NeST una njia nyingi za Ununuzi kulingana na uhitaji wa huduma au bidhaa husika suala ambalo linaupa mfumo sifa ya ukidhi na kuendana na uhitaji wa watumiaji wake.

“Waheshimiwa Wajumbe niwahakikishie kuwa, pamoja na kwamba tunaendelea na ujenzi wa mfumo wetu, ila tulipofikia mpaka sasa, Hatuna sababu ya kutotumia Mfumo, na kwamba Mfumo wa NeST unatosha” alisisitiza Mkurugenzi Simba na kumalizia.

Utoaji wa Zabuni kupitia Mfumo wa NeST ulianza rasmi mwezi Julai, 2023 ambapo mpaka sasa jumla ya zabuni zilizotangazwa kupitia NeST ni 90,959, huku tuzo za zabuni 69,806 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 4.28 zimetolewa kwa wazabuni mbalimbali kupitia bidhaa, kazi za ujenzi na huduma mbalimbali.

Ziara hiyo iliambatana na Kamati hiyo kwenda kutembelea timu ya wataalamu wa ujenzi wa Mfumo huo ambao wameweka kambi kituoni cha VETA Arusha ili kukamilisha sehemu ndogo ya moduli zilizobaki ambazo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wapili 2025.

 

Post a Comment

0 Comments

KAMATI YA BUNGE SHERIA YAPONGEZA MAENDELEO YA MATUMIZI YA NeST