WAZIRI MHAGAMA AWATAKA WATENDAJI KUSIMAMIA SHERIA ZA AFYA APASAVYO


📍Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria chapungua nchini.

📍Mkoa wa Tabora unaongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria.

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

WATENDAJI ngazi zote kuanzia ngazi ya Taifa, mikoa na Halmashauri wametakiwa kuhakikisha wanasimamia kwa dhati Sheria ipasavyo kupitia usimamizi wa Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 na sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni na miongozo iliyopo ili kuweze kudhibiti ugonjwa hatari wa malaria.

Takwimu hapa nchini zinaonesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kimepungua kwa takribani asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.

Hayo ameyasemwa leo Aprili 25,2025 jijini hapa na Waziri wa Afya Jenista Mhagama wakati akitoa tamko katika siku ya Malaria Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Aprili 25,amesema hiyo itawezesha kudhibiti mbu waenezao magonjwa mbalimbali wakiwemo waenezao malaria.

Amesema katika kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za malaria hapa nchini Wizara, imeimarisha na kuongeza msisitizo wa utekelezaji wa mikakati na afua zote za kupambana na malaria. 

Waziri huyo amefafanua kuwa msisitizo mkubwa kwa sasa unawekwa kwenye uwekezaji katika udhibiti wa mbu waenezao malaria kwa njia jumuishi ikiwemo kutoa kipaumbele katika afua ya usimamizi na udhibiti wa mazingira ili kuzuia mbu kuzaliana kwa kusimamia usafi wa mazingira na unyunyiziaji wa viuadudu vya Kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu. 

Ameeleza kuwa siku ya malaria duniani, huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili ambapo katika siku hii, Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha kumbukumbu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Waziri huyo amesema siku hiyo inalenga katika kutathmini utekelezaji wa mikakati na afua za za kudhibiti ugonjwa wa malaria, mafanikio yaliyopatikana kutokana na jitihada za Serikali na wadau, pamoja na changamoto zilizopo na jinsi ya kukabiliana nazo.

"Siku hii pia hutumika kutoa elimu na hamasa zaidi kwa jamii juu ya afua pendekezwa na wajibu wa makundi mbalimbali katika kupambana na malaria hapa nchini," ameongeza.

"Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu inasema “Malaria Inatokomezwa na Sisi: Wekeza, Chukua Hatua - Ziro Malaria Inaanza na Mimi.” Kauli mbiu hii inalenga katika kusisitiza kuongeza uwekezaji wenye tija katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria hapa nchini na umuhimu wa kila mmoja kuchukua hatua stahiki na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kuelekea malengo ya kuutokomeza ifikapo mwaka 2030," amesema.

Ameeleza kuwa takwimu hizo zinaonesha Mkoa wa Tabora unaongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria kwa asilimia 23, ukifuatiwa na Mkoa wa Mtwara wenye kiwango cha maambukizi asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mkoa wa Mara wenye asilimia 15.

Post a Comment

0 Comments

NAIBU WAZIRI MWANAIDI: TUNAKUSHUKURU RAIS DK.SAMIA KWA NYONGEZA YA MISHAHARA