Na Asha Mwakyonde,Dar es Salaam
MAMALAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imewezesha watu wenye ulemavu kupata stadi na kujikwamua kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yakiwamo ufundi cherehani na uchoraji wa ramani za majengo.
Watu hao wa makundi maalum wenye ulemavu wa viungo walisema kuwa hawakuona sababu ya kutokufanya kazi ya kuwaingizia kipato.
Joseph Mtei, Abdi Kipara, Gonsalva Lungu na Riziki Ndumba wenye ulemavu wa viungo ni mafundi ambao wamekuwa kivutio katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (maarufu kama Sabasaba) kutokana na umahiri walionao wa kufanya shughuli zao za kuwaingizia kipato.
Mtei ambaye anatumia miguu kuandika ni mwanafunzi wa fani ya uchoraji ramani katika Chuo cha Veta Dodoma wakati Kipara ambaye ni mhitimu wa Veta Singida pamoja Gonsalva na Riziki wahitimu wa Veta Songea wao wamekibobea katika ushonaji nguo.
Faulata Mutalemwa na Kintu Kilanga ambao ni Wakufunzi wa Veta, wamesema ufundi stadi unamwezesha mtu yeyote kuweza kujitegemea na kushauri jamii kutowaficha watu wenye ulemavu kwani wana uwezo mkubwa.
0 Comments