Na Asha Mwakyonde, Dar es Salaam
KAMISHNA Mkazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Zanzibar, Khatib Mwinyichande, ameeleza kuwa Uchaguzi Mkuu sio tukio la kisiasa pekee, bali ni jambo linalogusa haki za msingi za wananchi, kwa kuwa nchi ni ya kidemokrasia, viongozi hupatikana kupitia uchaguzi huru na wa haki.
Hayo ameyasema leo Julai 3,2025 jijini Dar es Salaam katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam 2025, ‘Saba Saba' amesema jukumu kuu la Tume hiyo ni kuhakikisha misingi ya kisheria na haki za binadamu zinalindwa katika kila hatua ya uchaguzi pamoja kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Amesema kuwa hilo linaloifanya THBUB kua na nafasi ya moja kwa moja katika mchakato wa uchaguzi na kwamba ina nafasi ya kipekee ya kikatiba katika kuhakikisha uchaguzi mkuu nchini unakuwa huru, haki na unaozingatia misingi ya utawala bora.
Kamishna huyo ameeleza katika kila hatua ya uchaguzi, Tume hiyo inachunguza, inabaini changamoto ,mapungufu na kuyawasilisha kwa mamlaka ya uchaguzi kwa ajili ya marekebisho kwenye uchaguzi unaofuata huku akisema hiyo ni njia mojawapo ya kulinda haki za wananchi.
"THBUB itakuwa miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi kuanzia kampeni, hadi siku ya kupiga kura, huku akisisitiza kuwa Tume itakuwa ikifuatilia mwenendo wa uchaguzi na kuandika ripoti itakayowasilishwa kwa mamlaka husika," amesema.
Ameongeza kuwa ushiriki wa Tume hiyo kwenye maonyesho hayo ni sehemu ya kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu haki, wajibu na namna ya kuishi kwa kuheshimu sheria na misingi ya demokrasia.
Amesema elimu hiyo inawasaidia wananchi kufahamu kuwa haki zao zinalindwa kisheria, huku akisema Tume ipo kwa ajili ya kuhakikisha k hakuna mwananchi anayebaguliwa au kunyimwa haki zake kwa misingi yoyote.
Mwinyichande amebainisha kuwa maonyesho haya yanawawezesha kukutana moja kwa moja na wananchi, kupokea malalamiko yao, kutoa elimu ya haki za binadamu, na kuwaeleza kuwa wao ni watetezi wao pale wanapokwazwa na kukosa haki zao.
0 Comments