📍Serikali kuimarisha uwezeshaji wa wahitimu wa vifungo kujitegemea
Na Asha Mwakyonde, DODOMA
JESHI la Magereza nchini limesema kuwa limepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya urekebishaji wa wafungwa kwa kuwapatia elimu, mafunzo ya ufundi stadi na ujuzi mbalimbali unaowawezesha kurejea katika jamii wakiwa raia wema na wenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Juni 18,2026 na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo ACP Elmas Mgimwa wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kitaifa, ambapo taasisi mbalimbali za Umma zinatoa elimu kuhusu huduma wanazozitoa kwa wananchi.
Amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa Jeshi la Magereza kuwaeleza wananchi kuhusu mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika mfumo wa magereza, ambao kwa sasa umejikita zaidi katika urekebishaji na maandalizi ya wafungwa kurejea katika jamii wakiwa watu wenye maadili mema na mchango chanya kwa Taifa.
Amefafanua kuwa historia ya magereza ilianza wakati wa ukoloni ambapo jukumu lake kuu lilikuwa ni kuwahifadhi wafungwa, lakini baada ya uhuru mfumo huo umebadilika na kuzingatia zaidi urekebishaji wa tabia na maendeleo ya wafungwa.
Kwa mujibu wake, hatua ya kwanza ni kupokea na kuhifadhi wafungwa kwa mujibu wa sheria, huku hatua inayofuata ikiwa ni kuwawezesha kupata elimu na mafunzo mbalimbali ikiwemo ufundi stadi, kilimo, ujasiriamali na stadi nyingine za maisha zinazowawezesha kujitegemea wanapomaliza vifungo vyao.
ACP Mgimwa ameeleza kuwa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu na mafunzo linaendelea kuwajengea uwezo wafungwa ili wanapotoka gerezani wawe tayari kuanza maisha mapya na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
“Lengo letu ni kuhakikisha mtu anayemaliza kifungo anakuwa amerekebika, amepata maarifa na ujuzi wa kumwezesha kuwa raia mwema na mwenye manufaa kwa familia yake na taifa kwa ujumla,” amesema.
Aidha, amewahimiza wananchi kutembelea banda la Jeshi la Magereza katika maonesho hayo ili kujionea huduma na programu mbalimbali zinazotekelezwa na jeshi hilo pamoja na kupata uelewa sahihi kuhusu dhana ya urekebishaji wa wafungwa.
Amesisitiza kwamba jamii inapaswa kuwapokea na kuwaunga mkono wafungwa wanaomaliza vifungo vyao badala ya kuwanyanyapaa, kwa kuwa wengi wao hutoka magerezani wakiwa wamepata mafunzo na kuandaliwa kuwa raia wema.
“Tunawaomba wananchi watambue kuwa mtu anapopelekwa gerezani kwa mujibu wa sheria hupitia mchakato wa kurekebishwa.
Anaporudi katika jamii anahitaji kupokelewa na kupewa nafasi ya kuanza maisha mapya,” amesema ACP Mgimwa.
Kamishna huyo pia ameeleza kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha wafungwa wanaomaliza vifungo kujitegemea kiuchumi kupitia mfuko maalumu unaotarajiwa kusaidia utekelezaji wa programu za urekebishaji.
Amesema mfuko huo utasaidia wahitimu wa vifungo waliopata mafunzo mbalimbali kupata mitaji au vifaa vya kuanzia kazi kulingana na taaluma walizojifunza wakiwa magerezani, ikiwemo useremala, ujenzi na fani nyingine za ufundi.
Kwa mujibu wake, hatua hiyo itasaidia kupunguza uwezekano wa wahitimu wa vifungo kurejea tena katika makosa na badala yake kuwa sehemu ya nguvu kazi inayochangia maendeleo ya taifa.
Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza linaendelea kufuatilia maendeleo ya baadhi ya wafungwa waliomaliza vifungo ili kujiridhisha kuwa wanatumia vyema elimu na ujuzi walioupata na kuendelea kuishi maisha yenye tija katika jamii.





0 Comments