Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amempongeza mhitimu wa fani ya uchoraji ramani za majengo kutoka Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Dodoma, Joseph Mtei, ambaye ni mtu mwenye ulemavu wa mikono anayebuni ramani za majengo na samani kwa kutumia miguu kupitia kompyuta mpakato.
Kikwete ametoa pongezi hizo leo Juni 17, 2026, alipotembelea banda la VETA katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, ambapo alishuhudia Mtei akitumia miguu yake kubuni ramani za majengo pamoja na samani za matumizi ya majumbani na hotelini kwa kutumia kompyuta mpakato.
“Nimefurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na VETA kupitia mafunzo yake. Tunaona vijana wetu wanavyobuni bidhaa zenye viwango kwa kutumia malighafi za ndani na kuzalisha bidhaa zinazotumika hata katika hoteli za kitalii,” alisema Kikwete.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni Tanzu ya VETA ya Ujuzi, Mhandisi Marco Kapinga, amesema kampuni hiyo imewahi kushinda tuzo ya watengenezaji bora wa samani kupitia ubunifu wa mhitimu huyo katika Tuzo za Zanzibar Awards zilizofanyika mwaka uliopita.
Amesema samani zinazobuniwa na Mtei zimekuwa zikiuzwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar na Arusha, hususan katika hoteli za kitalii.
“Hii ni sehemu ya juhudi za kuendeleza vijana wenye mahitaji maalum. Joseph alisoma VETA na baadaye akaajiriwa katika Kampuni ya Ujuzi Limited, ambayo huzalisha bidhaa mbalimbali. Ameonyesha uwezo mkubwa na ubunifu unaotambulika ndani na nje ya nchi,” alisema Mhandisi Kapinga.



0 Comments