VETA PWANI YATENGENEZA JOKOFU LA KUHIFADHI PARACHICHI KWA MUDA MREFU


 Na Asha Mwakyonde, DODOMA

CHUO cha Ufundi Stadi (VETA) Pwani kimebuni jokofu maalumu la kuhifadhia zao la parachichi linaloweza kuongeza muda wa uhifadhi wa mazao hayo na kupunguza upotevu unaowakumba wakulima baada ya mavuno.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, mwalimu wa fani ya utengenezaji majokofu na viyoyozi kutoka VETA, Haji Sinani amesema ubunifu huo ulitokana na maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, baada ya kutembelea mikoa inayozalisha parachichi kwa wingi na kubaini changamoto kubwa ya kuharibika kwa mazao hayo baada ya kuvunwa.

Amesema baada ya kupokea maelekezo hayo, wataalamu wa VETA kwa kushirikiana na ofisi za kanda walibuni jokofu hilo na kufanya majaribio yaliyobaini kuwa lina uwezo wa kuhifadhi parachichi kwa muda mrefu huku likidumisha ubora wake.

"Jokofu hili litawasaidia wakulima kutunza mazao yao kwa muda mrefu bila hofu ya kuharibika wakati wakisubiri kuyauza katika soko la ndani au nje ya nchi," amesema.

Amefafanua kuwa parachichi mabichi yanaweza kuhifadhiwa kwa muda wa kati ya miezi mitatu hadi mwaka mmoja, huku yale yaliyoiva yakidumu kati ya wiki mbili hadi mwezi mmoja, hali itakayowaongezea wakulima fursa ya kupata masoko yenye bei nzuri.

Aidha, amesema mfumo wa jokofu hilo umeundwa kudhibiti kiwango cha joto kati ya nyuzi joto 4 hadi 8 za Selsiasi, kiwango kinachofaa kwa uhifadhi wa parachichi, na kwamba teknolojia hiyo hujiendesha yenyewe kwa kuwasha na kuzima kulingana na kiwango cha joto kilichowekwa.

Ameeleza kwa sasa VETA ipo katika hatua za mwisho za majaribio ili kuhakikisha teknolojia hiyo inafanya kazi kwa ufanisi kabla ya kuanza kutumika kwa kiwango kikubwa na wakulima nchini.

Post a Comment

0 Comments

VETA SINGIDA YATOA TEKNOLOJIA YA SILAGE KUINUA UZALISHAJI WA MIFUGO