Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), kwa juhudi zake za kuboresha huduma kwa wakulima kupitia udhibiti wa afya ya mimea, matumizi salama ya viuatilifu na hatua mbalimbali zinazochangia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Dk. Nchemba alitoa pongezi hizo leo Agosti 1, 2026, alipotembelea banda la TPHPA wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 33 ya Siku ya Wakulima (Nanenane),yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Akiwa katika banda hilo, Waziri Mkuu alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, ambaye amemueleza kuwa mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha jitihada za kudhibiti baa la panzi, kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya viuatilifu na kulinda afya ya mimea ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Profesa Ndunguru amesema TPHPA pia inaendelea kutoa huduma za kitaalamu kwa wakulima nchini kwa lengo la kudhibiti visumbufu vya mazao, kuzuia kuenea kwa magonjwa ya mimea na kuhakikisha uzalishaji wa mazao unakuwa salama na wenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Akizungumza baada ya kupata maelezo hayo, Dk. Nchemba amesema utendaji wa TPHPA ni mfano wa utekelezaji wa kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane 2026 isemayo, "Tambua Soko, Zalisha kwa Tija Kutekeleza Dira ya 2050."
Ameelekeza mamlaka hiyo kuendelea kuboresha huduma zake, kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuimarisha utoaji wa elimu ili kuhakikisha mazao yanalindwa dhidi ya visumbufu na magonjwa, hatua itakayochangia kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa kilimo nchini.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuziunga mkono taasisi zinazotekeleza majukumu ya kulinda afya ya mimea kwa kuwa zina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa mazao, mapato ya wakulima na maendeleo ya sekta ya kilimo kwa ujumla.







0 Comments