Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),umewataka wananchi na wafanyabiashara wanaotumia majina tofauti na majina yao binafsi katika shughuli za biashara kuhakikisha wanayasajili kwa mujibu wa sheria, hatua ambayo itawalinda dhidi ya migogoro ya kisheria na matumizi yasiyo halali ya majina yao ya biashara.
Akizungumza leo Agosti 1, 2026 katika Maonesho ya Kilimo, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuf Mwasakafyuka, amesema ni kosa kwa mfanyabiashara kutumia jina tofauti na jina lake binafsi kuendesha biashara bila kulisajili rasmi.
Amesema, kwa mujibu wa sheria, mfanyabiashara anayefungua biashara kama saluni, duka au shughuli nyingine kwa jina tofauti anatakiwa kulisajili ndani ya siku 28 tangu aanze kulitumia.
"Mfanyabiashara haruhusiwi kutumia jina tofauti na jina lake binafsi kuendesha biashara bila kulisajili. Kwa mfano, ukifungua saluni na kuiwekea jina tofauti, unatakiwa ulisajili ndani ya siku 28.
"Usajili wa jina la biashara unasaidia kulinda biashara yako na kuzuia watu wengine kutumia jina hilo bila idhini," amesema Mwasakafyuka.
Ameeleza kuwa usajili wa jina la biashara humwezesha mmiliki kupata ulinzi wa kisheria wa jina analolitumia na kuzuia watu wengine kulitumia bila kibali.
Aidha, ameongeza kuwa sheria inampa Msajili mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya mtu anayekiuka utaratibu huo, ikiwemo kufuta usajili wa biashara husika, huku mhusika akiwajibika kwa madai ya fidia endapo matumizi ya jina hilo yatasababisha hasara kwa mmiliki halali.
Mwasakafyuka amewahimiza wafanyabiashara kuzingatia sheria za usajili wa majina ya biashara ili kulinda uwekezaji wao, kujiepusha na migogoro ya kisheria na kuhakikisha biashara zao zinafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

0 Comments