Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amelipongeza Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO),kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kuendeleza sekta ya uvuvi huku akisema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan unaifungua Tanzania kuingia kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu na kuimarisha uchumi wa buluu.
Hayo ameyasema leo Agosti 1, 2026 wakati alipotembelea banda la TAFICO katika Maonesho ya Nanenane 2026 ambayo yanafanyika Kitaifa jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nzuguni, Dk. Nchemba amesema sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta za kimkakati zinazobeba fursa kubwa za ajira, mapato na ukuaji wa uchumi, huku akibainisha kuwa dhamira ya Serikali ya kuinua sekta hiyo tayari inaonekana kupitia uwekezaji mkubwa uliofanyika katika bandari za uvuvi na vitendea kazi vya kisasa.
Aidha alilitaka shirika hilo kuendelea kusonga mbele na kuhakikisha linafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya taifa.
Awali akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa, amesema mafanikio yanayopatikana sasa yametokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
"Kwanza niishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika sekta ya uvuvi. Serikali imeendelea kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania kwa kulipatia meli za kisasa za uvuvi wa bahari kuu pamoja na kujenga bandari ya uvuvi ambayo itakuwa kitovu cha shughuli za uvuvi wa bahari kuu," amesema Matessa.
Ameeleza kuwa bandari hiyo itawezesha meli kushusha mazao ya uvuvi, kutoa huduma za uhifadhi na usafirishaji wa mazao hayo, pamoja na kuchochea ajira na shughuli nyingine za kiuchumi.
Matessa ameongeza uwekezaji huo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayolenga kuiwezesha Tanzania kuvua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone - EEZ), eneo ambalo kwa muda mrefu halijatumika ipasavyo kwa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.
Amebainisha kuwa kwa sasa TAFICO inamiliki meli moja ya uvuvi wa bahari kuu na maandalizi yanaendelea ya kushirikiana na sekta binafsi katika shughuli za uvuvi, huku Serikali ikiendelea na mpango wa kuongeza meli nyingine.
"Tupo katika hatua za kupata meli nyingine mbili hivi karibuni na baadaye zitanunuliwa nyingine, hivyo tutakuwa na meli nne za kuvua bahari kuu," amesema.
Matessa amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa TAFICO ipo tayari kutekeleza maelekezo yote ya Serikali kwa kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinatumika kwa tija, zinachochea ajira, zinaongeza mapato ya Serikali na kuvutia uwekezaji zaidi katika uchumi wa buluu.
Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko, Zalisha kwa Tija Kutekeleza Dira ya 2050."




0 Comments