IMELDA AISHINDA CHANGAMOTO YA ULEMAVU KUPITIA VETA


 📍Awapa moyo vijana wenye ulemavu kupitia VETA

Na Asha Mwakyonde, RUKWA

ULEMAVU haupaswi kuwa kikwazo cha mtu kutimiza ndoto zake, kwani kwa juhudi, mafunzo na mazingira wezeshi, kila mtu anaweza kutumia uwezo alionao kujenga maisha bora. Hilo linathibitishwa na Imelda Kanyengele, mwanafunzi mwenye ulemavu wa mkono anayesomea fani ya ushonaji katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Nkasi mkoani Rukwa.

Imelda, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili, amesema mafunzo anayopata chuoni hapo yamemwezesha kupata ujuzi wa kushona nguo za aina mbalimbali na kutengeneza batiki, hatua inayompa matumaini ya kujitegemea kiuchumi kupitia fani hiyo.

Akizungumza leo Oktoba 9,2026 katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo,” amesema alijiunga na VETA akiwa na matarajio ya kujifunza ujuzi ambao ungemsaidia kujiendeleza licha ya changamoto zinazoweza kuambatana na ulemavu wake.

“Katika chuo chetu nimejifunza mambo mengi, yakiwamo ushonaji wa nguo za aina mbalimbali. Sikutarajia kama ningefikia hatua hii, lakini sasa ninaweza kushona suruali, mashati na magauni, pamoja na kutengeneza batiki,” amesema.

Amesema mafunzo hayo yamemjengea uwezo na kujiamini katika fani ya ushonaji, huku akieleza kuwa mchango wa walimu wake umekuwa muhimu katika safari yake ya kujifunza na kupata ujuzi huo.

Imelda amewashukuru walimu wake kwa kumfundisha na kumsimamia vizuri, jambo lililomsaidia kuendelea kujifunza na kuboresha uwezo wake katika kazi za ushonaji.

Ameongeza kuwa ujuzi alioupata unamwezesha kushughulikia mahitaji ya wateja wa rika mbalimbali, hali inayompa matumaini ya kutumia taaluma yake kujipatia kipato na kujenga maisha ya kujitegemea.

Kwa kijana mwenye ulemavu wa mkono, kujifunza fani inayohitaji umakini na matumizi ya mikono ni hatua inayodhihirisha umuhimu wa kutoa fursa za mafunzo kwa watu wote, kwa kuzingatia uwezo wao na mazingira yanayowawezesha kushiriki kikamilifu.

Aidha, Imelda amewahimiza vijana wenzake, hususan wenye ulemavu, kutokata tamaa wala kujifungia nyumbani kwa kuhofia hali zao, badala yake wajitokeze kujiunga na vyuo vya VETA ili kupata ujuzi katika fani mbalimbali.

Amesema mafunzo ya ufundi stadi yanaweza kuwasaidia vijana kujiajiri, kuajiriwa na kutumia vipaji vyao kutengeneza fursa za kiuchumi, hivyo akawataka kuamini uwezo wao na kuchangamkia fursa zilizopo.

Imelda ametoa ujumbe kuwa vijana wenye ulemavu wanapaswa kupewa nafasi ya kujifunza na kuendeleza uwezo wao, kwani ulemavu hauondoi vipaji, ndoto wala nafasi ya mtu kuchangia maendeleo ya jamii.

Post a Comment

0 Comments

IMELDA AISHINDA CHANGAMOTO YA ULEMAVU KUPITIA VETA