JESHI LA ZIMAMOTO NA VETA KUSHIRIKIANA KUJENGA UJUZI WA UOKOAJI KWA VIJANA


 Na Asha Mwakyonde, RUKWA

VIJANA wametakiwa kuwa mabalozi wa usalama katika jamii zao kwa kutoa elimu ya kinga dhidi ya majanga ya moto na namna ya kukabiliana na dharura, ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na majanga hayo.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 10,2026 na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Rukwa, Mrakibu Msaidizi Chacha Mchaka, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika Wilaya ya Sumbawanga mkoani humo yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, Tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo,”.

Mchaka amesema jeshi hilo lipo tayari kushirikiana na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),katika kuendeleza ujuzi wa vijana, kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ya kutaka taasisi hizo kushirikiana.

Amesema jeshi hilo litakutana na viongozi wa VETA ili kujadili maeneo ya ushirikiano yatakayowawezesha vijana kupata elimu na ujuzi kuhusu masuala ya zimamoto na uokoaji.

Aidha, amesema kupitia banda lao katika maonesho hayo, wanatoa elimu kuhusu namna ya kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto, ukaguzi wa majengo pamoja na matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto.

Ameongeza kuwa wanawakaribisha vijana na wananchi kutembelea banda hilo ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na jeshi hilo, kazi zake na vifaa vinavyotumika katika shughuli za uokoaji na uzimaji moto.

Amesisitiza kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kusaidia kulinda maisha na mali za wananchi kwa kutumia maarifa watakayopata na kuyasambaza katika maeneo wanayoishi.

Akizungumzia maandalizi ya kukabiliana na athari za El NiƱo, Mchaka amesema Mkoa wa Rukwa uliendelea kutoa elimu kwa jamii wakati serikali ilipotangaza uwezekano wa kutokea kwa hali hiyo.

Amesema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira, kusafisha mitaro ya maji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.

Ameeleza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kuimarisha utayari wa jamii kukabiliana na majanga na kupunguza madhara yanayoweza kuepukika.

Post a Comment

0 Comments

REHEMA SOMBI ATEMBELEA MABANDA YA MAONESHO WIKI YA VIJANA RUKWA