Na Asha Mwakyonde, RUKWA
UKOSEFU wa ajira kwa vijana wenye ujuzi wa ufundi ni changamoto inayohitaji suluhisho linalowawezesha kutumia maarifa yao kujiajiri na kuanzisha biashara. Kupitia Mradi wa Skills for Entrepreneurship and Employability Development (SEED), vijana wanapata fursa ya kuimarisha ujuzi wao na kujiandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.
Mratibu wa mradi huo, Datius Tibaijuka, amesema SEED unaotekelezwa na Save the Children Tanzania na NMB Foundation, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), unalenga kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na mitaji kwa vijana.
Akizungumza leo Oktoba 10, 2026 mkoani Rukwa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, Tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo,” alisema mradi huo unawawezesha vijana na wakufunzi kupata ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko.
Amesema wakufunzi 39 kutoka vyuo vya VETA Chang’ombe, Kipawa na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni (FDC), pamoja na wanafunzi takribani 175, wanaendelea na mafunzo maalumu kupitia mradi huo.
Ameongeza kuwa mbali na mafunzo, vijana wanapatiwa vifaa vya kuanzia biashara (startup kits), elimu ya fedha na kuunganishwa na taasisi za fedha ili kuwawezesha kujiajiri na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Tibaijuka amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyuo vya ufundi, sekta binafsi na taasisi za fedha, akieleza kuwa elimu ya ufundi stadi ni nyenzo muhimu katika kupunguza ukosefu wa ajira na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa Kitengo cha Vijana kutoka Save the Children Tanzania, Lilian Kapinga, amesema taasisi hiyo inatekeleza miradi inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto katika jamii zao.
Ameutaja mradi wa Mchana Plus, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, kuwa unalenga kuimarisha taasisi za vijana kwa kuzipatia ruzuku na mafunzo ya kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kapinga akizungumzia mradi wa SEED, amesema mradi huo unalenga kuboresha uwezo wa wakufunzi wa VETA, kuwapatia wanafunzi ujuzi unaohitajika sokoni na kuwawezesha kwa vifaa vya kuanzia biashara pamoja na mafunzo ya ujasiriamali.
Kapinga amesema vijana wanapaswa kutambuliwa kama wadau muhimu wa maendeleo, wenye uwezo wa kujiajiri, kuajiri wengine na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.


0 Comments