PROF. MKENDA AIPONGEZA PPRA KUFUNGUA FURSA ZA ZABUNI KWA VIJANA


Na Asha Mwakyonde, RUKWA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia usajili wa makundi maalumu na upatikanaji wa zabuni za umma, akieleza kuwa hatua hiyo inachangia kuwawezesha vijana kujiajiri, kukuza mitaji na kujenga uwezo wa kujitegemea.

Prof. Mkenda ametoa pongezi hizo leo Oktoba 10, 2026 alipotembelea banda la PPRA katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika Rukwa, yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”

Kupitia fursa hizo, vijana wanaweza kushiriki katika shughuli za ununuzi wa umma kwa kuwania zabuni zinazotolewa na taasisi mbalimbali za serikali, hatua inayoweza kuwasaidia kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Akitoa maelezo kuhusu majukumu ya PPRA, Mkurugenzi wa Kuendeleza Uwezo wa Ununuzi wa mamlaka hiyo, Winifrida Samba, amesema mamlaka hiyo inasimamia ununuzi wa umma kwa kuhakikisha unazingatia taratibu na kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Amesema katika kutekeleza jukumu hilo, PPRA inahakikisha taasisi nunuzi zinatoa fursa za zabuni kwa makundi maalumu, hususan vijana, ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia mikataba ya serikali.

Samba ameeleza kuwa ushirikiano kati ya PPRA na Ofisi ya Rais inayoshughulikia Maendeleo ya Vijana, pamoja na kuingizwa kwa ajenda ya usajili wa makundi maalumu katika mbio za Mwenge wa Uhuru, umechangia kuongeza idadi ya makundi yanayosajiliwa.

Amesema kabla ya juhudi hizo kuimarishwa, jumla ya makundi maalumu 1,557 yalikuwa yamesajiliwa, yakiwamo makundi ya vijana 878 huku akifafanua kuwa wanawake ni 600, wazee 48 na watu wenye ulemavu 31.

Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa, hadi Oktoba 10, mwaka huu, jumla ya makundi ya

31,928 yalikuwa yamesajiliwa tangu Julai 2020, yakiwamo makundi ya vijana 15,165, wanawake 15,397, wazee 712 na Watu wenye ulemavu 654.

Katika upande wa upatikanaji wa zabuni, Samba amesema kuanzia Julai 2023 hadi Oktoba 10, mwaka huu, jumla ya zabuni 3,466 zilitolewa kwa makundi maalumu, zikiwa na thamani ya Shilingi bilioni 74.32.

"Makundi ya vijana yalipata zabuni 2,066 zenye thamani ya Sh bilioni 40.6, hali inayoonesha mchango wa fursa za ununuzi wa umma katika kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi, wanawake 1,264 zenye thamani ya shilingi bilioni 29. 

76, wazee 93 zenye thamani ya shilingi bilioni 3.36 na Watu wenye ulemavu 43 zenye thamani ya shilingi milioni 635. 7," amesema.

Amesisitiza kuwa PPRA itaendelea kusimamia eneo hilo ili kuhakikisha ununuzi wa umma unawanufaisha wananchi, hususan vijana, kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika zabuni na kujenga uwezo wa kuendesha biashara zao.

Aidha, amewahimiza vijana kujisajili kama makundi maalumu na kufuatilia matangazo ya zabuni yanayotolewa na taasisi za umma ili kutumia fursa zilizopo kukuza mitaji, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments

REHEMA SOMBI ATEMBELEA MABANDA YA MAONESHO WIKI YA VIJANA RUKWA