UVCCM YAWEKA MKAKATI KUVUTA VIJANA WENGI CCM

Na Asha Mwakyonde, RUKWA

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Rehema Sombi Omary, amewahimiza vijana kutumia fursa zinazotolewa na Chama cha Mapinduzi (CCM), kujiunga na chama hicho na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

Ameyasema hayo leo Oktoba 10,2026 wakati akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana mkoani Rukwa, yenye kaulimbiu isemayo “Tanzania ni yetu sote, Tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”akiwa katika banda la umoja huo.

Makamu Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa vijana ni vema vijana wakapata fursa ya kutembelea banda hilo na kujisajili kuwa wanachama wa CCM na kueleza changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi.

Rehema amesema kuwa usajili wa wanachama ni muhimu katika kukijenga chama hicho, huku akiwahimiza vijana ambao bado hawajajiunga kutumia fursa hiyo kuwa wanachama kamili na kushiriki katika shughuli za chama.

Amebainisha kuwa CCM imeendelea kuwa sehemu muhimu ya safari ya maendeleo ya Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia serikali zilizotokana na chama hicho.

Aidha, amesema Wiki ya Vijana inapaswa kuwa jukwaa la vijana kueleza kero zao, mahitaji na matarajio yao, ili viongozi na taasisi husika wapate nafasi ya kuzisikiliza na kutafuta suluhisho.

Amesema mabanda yaliyowekwa katika maadhimisho hayo yanatoa nafasi kwa vijana kuwasilisha changamoto zao, huku masuala yanayohitaji msaada wa chama yakiweza kufikishwa kwa viongozi husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Rehema amewataka vijana wa Rukwa na wananchi kwa ujumla kujitokeza kushiriki katika shughuli muhimu za kitaifa zinazotarajiwa kufanyika mkoani humo, akisema matukio hayo ni fursa ya kuonesha mshikamano na kuhamasisha maendeleo ya eneo hilo.

Ameeleza kuwa Rukwa ina nafasi ya kuendelea kupiga hatua za maendeleo kupitia ushiriki wa wananchi, hususan vijana, katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amewahimiza wanachama wa CCM kuendelea kujiandaa kwa michakato ya uchaguzi ndani ya chama, akieleza kuwa uchaguzi mmoja unapomalizika, maandalizi ya uchaguzi unaofuata huanza kwa kuzingatia taratibu za chama.

Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha umoja, kudumisha amani na kushiriki katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments

REHEMA SOMBI ATEMBELEA MABANDA YA MAONESHO WIKI YA VIJANA RUKWA