Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
MKUTANO wa 11 wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMnet) unaotarajiwa kufanyika Zanzibar umevutia mwitikio mkubwa kutoka ndani na nje ya Tanzania, baada ya idadi ya washiriki waliojiandikisha kufikia 1,200, kutoka makadirio ya awali ya watu 800.
Mwitikio huo unaashiria kuongezeka kwa hamasa ya wadau wa usimamizi wa rasilimaliwatu katika sekta ya umma barani Afrika kushiriki mkutano huo, huku maandalizi yake yakifikia asilimia 90 kuelekea ufunguzi wake katika Hoteli ya Verde, Zanzibar.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Rais wa APS-HRMnet, Xavier Daudi, amesema idadi ya waliojiandikisha imevuka matarajio ya awali, hali inayoonesha mwitikio mkubwa wa washiriki kutoka mataifa mbalimbali.
Ameeleza kuwa kuvutia kwa Tanzania, hususan Zanzibar, kumekuwa miongoni mwa sababu zinazochangia mwitikio huo, akibainisha kuwa eneo hilo lina vivutio vya utalii, usalama, ukarimu wa wananchi pamoja na mazingira yanayozingatia viwango vya kidiplomasia.
Daudi amebainisha kuwa zaidi ya nchi 20 za Afrika zinatarajiwa kuwakilishwa katika mkutano huo, zikiwemo kupitia ushiriki wa Mawaziri na Makatibu Wakuu wenye dhamana ya Utumishi wa Umma.
Aidha, amewataka washiriki kutoka ndani ya Tanzania kuanza kufika Zanzibar Novemba 8, 2026, kwa ajili ya kuchukua vifurushi vyao vya ushiriki, huku wale wanaotoka nje ya nchi wakitakiwa kufanya hivyo Novemba 9, 2026, katika eneo la mkutano, Hoteli ya Verde.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kukutanisha viongozi na wataalamu wa rasilimaliwatu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kwa ajili ya kujadili masuala ya usimamizi na maendeleo ya rasilimaliwatu katika sekta ya umma.










0 Comments