FCC YAZIHAMASISHA TAASISI ZA FEDHA KUFADHILI MIRADI YA MAENDELEO NA VIWANDA

DURBAN - AFRIKA KUSINI

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC),Khadija Ngasongwa, amezishauri nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuwekeza zaidi katika maendeleo ya viwanda na miundombinu ili kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Ngasongwa ametoa wito huo jijini Durban, Afrika Kusini, wakati akishiriki Mkutano wa Wiki ya Tisa ya Viwanda ya SADC unaoendelea nchini humo.

"Ushiriki wa FCC katika wiki hii unalenga kuhakikisha sera na miongozo ya ushindani wa haki inazingatiwa katika maendeleo ya viwanda. Tunataka kuona viwanda vya ukanda wetu vinakuwa na ushindani, vinatoa fursa kwa wanawake na vijana, na vinatoa bidhaa zenye ubora kwa walaji," alisema Bi. Ngasongwa.

Ameongeza kuwa uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya malighafi utasaidia kuwainua kiuchumi wanawake na vijana, kupanua masoko ya bidhaa za nchi za SADC na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Akizungumzia ushiriki wa Tanzania,  Ngasongwa amesema mkutano huo unaendana na vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania hususan katika sekta za madini, kilimo, bidhaa za afya, miundombinu na ubunifu.

"Ushiriki wa Tanzania una umuhimu mkubwa kwa sababu unajikita katika kuimarisha mnyororo wa thamani. Ni maeneo muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda na kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema.

Ngasongwa pia amewataka wadau wa fedha waliopo katika mkutano huo ikiwemo TIB, Exim Bank, BADEA na Nedbank kushirikiana katika kuhamasisha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi ya maendeleo na uwekezaji nchini.

Amehitimisha kwa kusema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya kimkakati na rasilimali nyingine. Hivyo ni muhimu kuyachakata ndani ya nchi badala ya kuuza malighafi ili kuongeza thamani, kuzalisha ajira na kuchochea ukuaji wa viwanda.

Mkutano wa Wiki ya Viwanda ya SADC ulifunguliwa rasmi Julai 27, 2026 na ulihitimishwa Julai 31, 2026 na umetoka na maazimio ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 46 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2026 Jijini Durban, Afrika Kusini.

Post a Comment

0 Comments

TFC YAHAMASISHA MATUMIZI YA MBOLEA KWA TIJA YA KILIMO