Na Asha Mwakyonde, TANGA
WAKATI teknolojia ikiendelea kubadili namna watu wanavyofanya kazi na kupata huduma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimechukua nafasi hiyo kama daraja la kuhakikisha elimu haifungwi na mipaka ya darasa, muda wala umbali, bali inamfuata mwanafunzi mahali alipo.
OUT imesema itaendelea kuwa kinara katika ubunifu wa utoaji wa elimu kwa njia huria na mtandao, kwa kutumia teknolojia na mifumo inayomwezesha mwanafunzi kusoma sambamba na shughuli zake za kila siku.
Akizungumza leo Agosti 24,2026 kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, Profesa Alex Makulilo, kiongozi wa timu ya OUT katika maonesho ya Wiki ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Manispaa ya Tanga, Dk. Straton Ruhinda amesema ubunifu ni sehemu muhimu ya mkakati wa Chuo kuhakikisha elimu inamfikia mwanafunzi popote alipo.
Amesema OUT imeendelea kubuni zana na mifumo mbalimbali ya kufundishia na kujifunzia inayomruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo bila ulazima wa kufika chuoni mara kwa mara.
“Chuo hiki kimekuwa kiongozi katika ubunifu wa zana na mifumo ya kufundishia na kujifunzia, kiasi kwamba mwanafunzi anaweza kusoma akiwa alipo bila kulazimika kufika chuoni mara kwa mara.
Wengine wanafika OUT wakati wa mahafali au baada ya kumaliza kabisa. Haya yote yanawezekana kutokana na ubunifu mkubwa uliowekezwa na Chuo,” amesema Dk. Ruhinda.
Ameelza kuwa mifumo hiyo imeondoa changamoto za umbali na muda, hivyo kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo huku wakiendesha kazi, biashara na majukumu mengine ya kila siku.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi, Dk. Rwejuna, amesema ubunifu katika elimu hauishii katika matumizi ya teknolojia pekee, bali unahusisha pia mbinu mpya za ufundishaji, ujifunzaji na utoaji wa huduma kwa wanafunzi.
Amesema OUT inaendelea kutumia TEHAMA, ujifunzaji kupitia mitandao, vifaa vya kidijitali na mifumo ya kisasa ya huduma za wanafunzi ili kuongeza ufanisi, ubora na upatikanaji wa elimu.
“Ubunifu unaiwezesha OUT kuwafikia wanafunzi waliopo katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya Tanzania bila kikwazo cha umbali. Teknolojia inamwezesha mwanafunzi kujifunza, kufanya mitihani, kupata huduma za kitaaluma na kuwasiliana na Chuo akiwa alipo,” amesema.
Ameongeza kuwa ubunifu huo pia unalenga kuhakikisha programu na mitaala ya Chuo inaendana na mahitaji ya jamii, soko la ajira pamoja na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa OUT, mwanafunzi ndiye kitovu cha huduma, huku ubunifu ukilenga kuhakikisha mahali alipo, muda alionao na majukumu yake haviwi kikwazo cha kupata elimu.
Kupitia ubunifu unaoendelea, OUT inalenga kuimarisha nafasi yake kama kinara wa elimu huria na mtandao nchini Tanzania na taasisi inayovuka mipaka ya kijiografia katika utoaji wa elimu, sambamba na kuchangia katika kujenga nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya karne ya 21.





0 Comments