MAHUNDI AWASHTUA VIJANA IWAMBI KUTUMIA MICHEZO KUPATA AJIRA, KUJENGA IWAMBI BILA UHALIFU


Na Mwandishi wetu, Mbeya 

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka amewataka vijana kutumia michezo kama fursa ya kujipatia ajira na kujenga maisha yao, huku wakiepuka vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi na ukatili wa kijinsia.

Naibu Waziri Mahundi ameyasema hayo wakayi akikabidhi vifaa vya michezo kwa timu 13 za Kata ya Iwambi jijini Mbeya.

Amesema michezo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwaweka vijana pamoja, kuwajengea vipaji na kuimarisha amani na mshikamano katika jamii huku akiwataka wananchi wa Iwambi kuunda timu moja imara itakayowakilisha kata hiyo katika mashindano mbalimbali na kuitangaza Iwambi kupitia michezo.

Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa klabu ya mbio za pole (jogging) katika kata hiyo, akisema mazoezi ni muhimu katika kuimarisha afya na kusaidia jamii kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwani michezo inapaswa kuwa chombo cha kuimarisha upendo na mshikamano ndani na nje ya Kata ya Iwambi, huku akitoa wito wa kushirikiana katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Iwambi, Groria Ipopo Mwamajemba (Mchina), amemshukuru Mahundi kwa msaada huo, akisema amekuwa sehemu ya wakazi wa Iwambi na ameendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo katika kata hiyo.

Mwamajemba amesema kupitia michezo, vitendo vya uhalifu vimepungua kwa kiasi kikubwa katika Kata ya Iwambi, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika michezo kwa vijana.

Mahundi ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Mkurugenzi wa Maryprisca Women Empowerment Foundation (MWEF), amekabidhi jozi mbili za vifaa vya michezo kwa kila timu pamoja na mpira mmoja kwa kila timu, katika hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Sekondari Iwambi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Diwani wa Kata ya Iwambi, Groria Ipopo Mwamajemba maarufu kama Mchina, aliyeanzisha mashindano ya mpira wa miguu yaliyowakutanisha vijana kutoka mitaa mbalimbali ya kata hiyo.







Post a Comment

0 Comments

MAHUNDI AWASHTUA VIJANA IWAMBI KUTUMIA MICHEZO KUPATA AJIRA, KUJENGA IWAMBI BILA UHALIFU