RAIS SAMIA AKABIDHI VYAMA VYA USHIRIKA MATREKTA


 📍Aagiza vyama vya ushirika kusimamia matrekta kwa tija

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amevitaka Vyama vya Ushirika nchini kusimamia ipasavyo matrekta na zana za kilimo wanazokabidhiwa, ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwafikia wakulima katika Kanda zao.

Amesema Serikali imeamua kutumia Vyama vya Ushirika kama njia muhimu ya kuwafikishia wakulima huduma za zana za kilimo, kutokana na kuwa karibu na wakulima na kufahamu mahitaji yao, hatua inayolenga kuongeza tija, uzalishaji na kipato cha wakulima.

Rais Samia ametoa msisitizo huo leo Agosti 8, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA),pamoja na Vyama vya Ushirika, katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dk.John Malecela, Nzuguni jijini hapa ambapo amesema Serikali ina imani na Vyama vya Ushirika katika kusimamia matrekta hayo na kuhakikisha yanawanufaisha wakulima.

“Sasa tunaanza na nyie, nitakabidhi matrekta yaliyopo hapa yaende yakafanye kazi. Tutaendelea kununua hadi tueneze kama tulivyoahidi,” amesema Rais Samia.

Amesema awali Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha vituo vya zana za kilimo katika Kanda mbalimbali nchini, lakini baada ya kutafakari namna bora ya kuwafikia wakulima, ilibaini kuwa Vyama vya Ushirika vina nafasi kubwa katika kusimamia huduma hizo.

Ameongeza kuwa Vyama vya Ushirika viko karibu na wakulima na vina uelewa wa mahitaji yao, hivyo vinaweza kuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha zana za kilimo zinawafikia walengwa na kutumika kuongeza uzalishaji.

“Nimezindua matrekta kwa ajili ya Vyama vya Ushirika. Mtakumbuka niliahidi kuanzisha vituo vya zana za kilimo katika Kanda zitakazokuwa ndani ya Tanzania nzima,” amesema.

Rais Samia amesema Serikali imekaa na kuamua utekelezaji wa mpango huo usimamiwe na Vyama vya Ushirika katika Kanda zao, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za zana za kilimo kwa wakulima.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Serikali itaendelea kukabidhi matrekta na zana nyingine za kilimo kwa Vyama vya Ushirika ili viweze kuzisimamia na kuhakikisha wakulima katika maeneo yao wanapata huduma hizo kwa wakati.

Amesisitiza kuwa matrekta na zana hizo zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuwasaidia wakulima kupunguza changamoto ya upatikanaji wa zana za kilimo, kuongeza tija na hatimaye kuongeza uzalishaji na kipato.

“Tumewakabidhi matrekta haya na zana tutakazonunua kwa Vyama vya Ushirika ili wao wawasimamie wakulima wao,” amesema Rais Samia.

Post a Comment

0 Comments

FCC YAIMARISHA ELIMU YA USHINDANI NA ULINZI WA WALAJI