MARANYA ENGINEERING YABUNI MASHINE ZA KUCHAKATA MABAKI YA MAZAO KUWA CHAKULA CHA MIFUGO

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

UBUNIFU wa teknolojia za ndani unaendelea kutoa suluhisho kwa changamoto za kilimo na ufugaji nchini, huku kampuni ya Maranya Engineering and Metals Limited ikibuni mashine zinazochakata mabaki ya mazao na taka za masokoni kuwa chakula bora cha mifugo, hatua inayolenga kupunguza gharama za ufugaji, kuongeza tija ya uzalishaji na kulinda mazingira.

Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane 2026, Mwanzilishi wa Maranya Engineering Limited amesema kampuni hiyo ilianzishwa baada ya kupata mafunzo ya ufundi na kujiajiri, kutoka Chuo cha VETA Dar es Salaam ambapo kwa sasa inaendesha shughuli zake katika eneo la Chanika, jijini humo.

Amesema kampuni hiyo imebobea katika utengenezaji wa mashine mbalimbali za kilimo na usindikaji wa mazao, ikiwemo mashine za kuchakata chakula cha mifugo, mashine za kusindika nafaka kama karanga, korosho na ufuta pamoja na mashine za kutengeneza siagi ya karanga (peanut butter).

Ameeleza kuwa mashine za kutengeneza chakula cha mifugo zimebuniwa ili kutumia mabaki ya mazao na taka za masokoni kama mboga mboga, majani, karoti, mahindi, makapi na malighafi nyingine ambazo mara nyingi hutupwa, na kuzigeuza kuwa chakula chenye virutubisho kwa mifugo.

Kwa mujibu wake, teknolojia hiyo inasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za kikaboni, huku ikiwapa wafugaji fursa ya kupata chakula cha mifugo kwa gharama nafuu.

Ameeleza matumizi ya chakula hicho huongeza afya ya mifugo, huimarisha uzalishaji wa maziwa na mayai, huongeza uzito wa mifugo na kupunguza gharama za ulishaji ambazo ni sehemu kubwa ya gharama za ufugaji.

Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya malighafi zinazotumika, ikiwemo maganda ya papai, vitunguu saumu na majani ya mwarobaini, vina uwezo wa kusaidia kuongeza kinga ya mifugo dhidi ya baadhi ya magonjwa na kuboresha afya ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.

Amewahimiza wakulima, wafugaji na wawekezaji kutembelea banda la Maranya Engineering katika Maonesho ya Nanenane ili kujionea teknolojia mbalimbali zinazotengenezwa na kampuni hiyo na namna zinavyoweza kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo na mifugo.

Ameongeza kuwa Maranya Engineering Limited ipo tayari kutengeneza mashine kulingana na mahitaji ya mteja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau wote wanaotaka kuwekeza katika teknolojia za usindikaji wa mazao na utengenezaji wa chakula cha mifugo.

Post a Comment

0 Comments

COPRA YAJA NA JARIDA LA THAMANI KUSUKUMA TAARIFA NA FURSA ZA MAZAO