Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imezindua Jarida la Thamani litakalotumika kutoa taarifa kuhusu shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo pamoja na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mazao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jarida hilo, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, amesema jarida hilo litachapishwa mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kuwafikishia wadau taarifa kuhusu kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo pamoja na mabadiliko yanayotarajiwa katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao.
Mlola amesema jarida hilo litakuwa jukwaa la kuonesha thamani ya shughuli zinazofanywa na COPRA, sambamba na kutoa elimu kuhusu udhibiti wa ubora, uzalishaji na fursa za biashara ya mazao.
Amesema uzinduzi wa jarida hilo ni sehemu ya jitihada za COPRA za kuendelea kusambaza taarifa kwa wadau wa ndani na nje ya taasisi, ili kuongeza uelewa na ushiriki katika sekta ya mazao.

0 Comments