TPHPA YATUMIA TEKNOLOJIA YA JUU KUBAINI VISUMBUFU VYA MAZAO

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imeanza kutumia teknolojia ya kisasa ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kubaini visumbufu vya mazao, hatua inayolenga kuwawezesha wakulima kutumia viuatilifu sahihi kulingana na aina ya kisumbufu kilichobainika.

Teknolojia hiyo imefanyiwa majaribio kupitia sampuli zilizochukuliwa katika mashamba ya wakulima katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, ambapo sampuli za mazao mbalimbali zikiwemo mihogo, vitunguu, karanga, sukuma wiki, chinese na beetroot zilichunguzwa.

Akizungumza leo Agosti 8,2026 wakati wa kuwasilisha matokeo ya uchunguzi huo, katika banda la mamlaka hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, amesema matumizi ya teknolojia hiyo yataondoa tabia ya wakulima kutumia viuatilifu kwa kubahatisha, jambo ambalo limekuwa likiongeza gharama za uzalishaji na kuhatarisha mazingira.

Amesema teknolojia hiyo inaweza kubaini bakteria, virusi, fangasi pamoja na visumbufu vingine hata pale ambapo mmea haujaonyesha dalili zinazoonekana kwa macho.

“Lengo ni kwamba kama ni bakteria ambaye udhibiti wake unahitaji kutumia kiuatilifu, tutakwenda na kiuatilifu sahihi, si tena kukisia,” amesema Profesa Ndunguru.

Kwa mujibu wa Prof. Ndunguru, katika zao la mihogo walibainika visumbufu mbalimbali, ikiwemo utitiri, bakteria na fangasi, huku baadhi ya visumbufu hivyo vikionekana kuwa na uwezo wa kudhoofisha mimea na kusababisha madhara zaidi.

Amesema katika zao la vitunguu vilibainika visumbufu vinane, vikiwemo bakteria na fangasi, huku matokeo yakionyesha kuwa sehemu kubwa ya visumbufu vilivyobainika vilikuwa vya bakteria.

“Uzuri wa teknolojia hii ni kwamba hata kama kuna kisumbufu ndani ya mmea na mmea hauonyeshi dalili yoyote, teknolojia hii itakuonyesha. Hii itasaidia sana katika udhibiti,” amesema.

Ameongeza kuwa teknolojia hiyo pia inaweza kuwa muhimu katika udhibiti wa usafirishaji wa mbegu kutoka eneo moja kwenda jingine, kwa kuwa inaweza kubaini uwepo wa vimelea ndani ya mbegu hata kama hazionyeshi dalili za ugonjwa.

Katika zao la karanga, amesema visumbufu vitatu vilibainika, ikiwemo virusi vinavyoweza kuathiri mfumo wa mmea wa kutengeneza chakula na kusababisha majani kuwa ya njano pamoja na kudumaa kwa mimea.

Kwa upande wa chinese, visumbufu sita vilibainika, vikiwemo bakteria na fangasi, huku baadhi vikihusishwa na kusababisha kuoza kwa mimea.

Aidha, katika zao la sukuma wiki, teknolojia hiyo ilibaini aina tatu za visumbufu, ambavyo ni bakteria, fangasi na virusi.

Prof. Ndunguru amesema TPHPA inalenga kuendelea na uchunguzi huo katika maeneo mbalimbali nchini ili kupata takwimu pana zitakazowezesha kutengeneza ramani ya kitaifa inayoonyesha aina na usambazaji wa visumbufu vya mazao katika maeneo mbalimbali.

Amesema ramani hiyo itasaidia kuwezesha usambazaji wa viuatilifu kwa njia ya kimkakati, kwa kupeleka kiuatilifu sahihi katika eneo sahihi kwa ajili ya kudhibiti kisumbufu kilichobainika.

“Tutakapofanya mchakato huu nchi nzima, tutatengeneza ramani itakayoonyesha visumbufu vilivyopo, vipo wapi na kwa kiwango gani. Hivyo, wakati wa kudhibiti, usambazaji wa viuatilifu utakuwa wa kimkakati,” amesema.

Amesema hatua hiyo itawezesha udhibiti endelevu wa visumbufu vya mazao, kuongeza uzalishaji, kufungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi, kuongeza ajira na kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni.

Prof. Ndunguru amesema matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija na kukuza uchumi wa nchi, akieleza kuwa teknolojia hiyo inafanya uchunguzi wa moja kwa moja kwenye DNA ya kisumbufu na hivyo kutoa matokeo yenye uhakika.

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Salum Ally, amesema matumizi ya teknolojia hiyo yamewasaidia wataalamu kupata taarifa ambazo awali hazikuweza kubainika kwa kutumia uchunguzi wa macho pekee.

Amesema awali wakulima walikuwa wakitumia uzoefu wa matatizo waliyokutana nayo katika misimu iliyopita kuamua aina ya dawa ya kutumia, hali ambayo wakati mwingine ilisababisha tatizo kuendelea kwa sababu chanzo halisi hakikubainika.

“Kupitia kipimo hiki sasa tunafungua macho zaidi kuhusu changamoto ambazo kwa macho yetu hatukuweza kuziona, ili tuweze kuwasilisha ujumbe wa moja kwa moja kuhusu tiba sahihi,” amesema Ally.

Amesema teknolojia hiyo itawasaidia wataalamu kutoa ushauri sahihi kwa wakulima na kuwawezesha kuzalisha katika mazingira salama yasiyoathiriwa na visumbufu vya mazao.

Ameishauri TPHPA kuangalia namna ya kuifikisha teknolojia hiyo kwa wakulima wengi zaidi nchini ili waweze kunufaika na matokeo ya uchunguzi na kuongeza tija katika uzalishaji.

Post a Comment

0 Comments

FCC YAIMARISHA ELIMU YA USHINDANI NA ULINZI WA WALAJI