Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MFUKO wa SELF Microfinance Fund (SELF MF),umewahimiza vijana, wajasiriamali, wakulima, wafugaji na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko huo ili kujiajiri, kuanzisha viwanda vidogo, kuongeza thamani ya mazao na kuwekeza katika biashara zinazochochea matumizi ya nishati safi, hatua inayolenga kuongeza ajira, kukuza uzalishaji na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Wito huo umetolewa leo Agosti 5, 2026 katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma na Meneja Masoko na Uhamasishaji wa SELF Microfinance Fund, Linda Mshana.
Mshana amesema mfuko huo umejikita katika kutoa elimu ya fedha sambamba na mikopo inayowawezesha wananchi kuanzisha na kukuza shughuli mbalimbali za uzalishaji, hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Amesema mbali na kuwawezesha wajasiriamali waliopo, SELF MF pia inatoa fursa kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara mpya, ikiwemo biashara ya kahawa, usindikaji wa mazao pamoja na biashara zinazohusiana na nishati safi kama uzalishaji na uuzaji wa majiko banifu.
"Tunawahamasisha vijana kutumia fursa zilizopo. Unaweza kujifunza kutengeneza kahawa au bidhaa nyingine, kupata mkopo na kuanzisha biashara yako. Hii inachangia kuongeza ajira, kukuza kilimo cha kahawa na kuongeza thamani ya mazao ya ndani," amesema Mshana.
Ameongeza kuwa mfuko huo unaendelea kuunga mkono juhudi za matumizi ya nishati safi kwa kufadhili biashara na shughuli zinazochangia utunzaji wa mazingira, huku ukiwawezesha wananchi kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo kuanzia uzalishaji, uchakataji, usafirishaji hadi masoko.
Kwa mujibu wa Mshana, SELF Microfinance Fund tayari imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa wanufaika mbalimbali nchini, ambapo zaidi ya wananchi laki sita wamenufaika na huduma hizo, huku lengo likiwa kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Amefafanua kuwa masharti ya kupata mkopo ni rafiki, ambapo mwombaji anatakiwa kuwa na shughuli ya uzalishaji au biashara iliyodumu kwa angalau mwaka mmoja ili kustahili kupata huduma hiyo.
Mbali na mikopo, amesema mfuko huo pia unatoa elimu ya fedha inayowasaidia wananchi kupanga uwekezaji, kukuza mitaji, kutumia mikopo kwa ufanisi na kuepuka madeni yasiyo ya lazima.
Aidha, amesema SELF MF hutoa huduma za bima, ikiwemo bima ya usafirishaji wa mazao na bidhaa, inayolinda mali za wafanyabiashara dhidi ya hasara zinazoweza kujitokeza wakati wa usafirishaji.
Amewataka wananchi kutembelea banda la SELF Microfinance Fund katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu, ushauri na kufahamu fursa mbalimbali za mikopo pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na mfuko huo kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi.

0 Comments