MASHINE ZA KITANZANIA ZAVUKA MIPAKA, ZAWAFIKIA WAKULIMA NJE YA NCHI


📍Ubunifu, uwekezaji na teknolojia vyaifanya Imara Teknolojia Ltd kuwa nguvu mpya ya kilimo

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

KUTOKA wazo lililoanzia kwenye utafiti na ubunifu mdogo hadi kuwa kampuni inayozalisha mashine za kilimo zinazotumiwa na zaidi ya wakulima laki moja ndani na nje ya Tanzania, safari ya Imara Teknolojia Ltd inaonyesha namna ubunifu na uwekezaji katika teknolojia unavyoweza kubadili sekta ya kilimo na kuongeza fursa za kiuchumi.

Kampuni hiyo imeendelea kuwa chachu ya mapinduzi katika kilimo kwa kuzalisha mashine mbalimbali zinazomsaidia mkulima kuongeza ufanisi wa uzalishaji, ikiwemo mashine inayoweza kuchakata mazao aina tisa tofauti pamoja na mashine za kutengeneza chakula cha mifugo.

Akizungumza katika Maonesho ya 33 ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dk. John Malecela Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Imara Teknolojia Ltd, Alfred Chengula, anasema kampuni hiyo ilianza mwaka 2015 ikiwa ni wazo la ubunifu kabla ya kupata msaada wa ruzuku kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), uliowezesha kutengeneza mfano wa kwanza wa mashine.

Anasema baada ya kutengeneza mashine hiyo na kufanya majaribio, kampuni ilipata ruzuku nyingine kutoka COSTECH kwa ajili ya kufanya utafiti wa soko na kubaini mahitaji ya wakulima kabla ya kuingia rasmi sokoni.

“Tulianza rasmi mwaka 2019 tukiwa watu watatu ambao ni wabunifu, hadi sasa tumefanikiwa kuwa na wafanyakazi zaidi ya 50 na tumeshazalisha na kusambaza zaidi ya mashine ndani na nje ya nchi,” anasema Chengula.

Anaeleza kuwa mashine zinazozalishwa na kampuni hiyo zimefikia nchi mbalimbali ikiwemo Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda, Zimbabwe, Malawi na Kenya, huku jumla ya mashine zaidi ya 300 zikiwa zimeuzwa nje ya Tanzania.

Chengula anasema mashine yao kuu inaweza kuchakata mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, maharage, mtama, mbaazi, alizeti, choroko na uwele, jambo linaloifanya kuwa tofauti na mashine nyingine zinazofanya kazi moja pekee.

Aidha, anaongeza kuwa kampuni hiyo pia inazalisha mashine maalumu ya kutengeneza chakula cha mifugo inayoweza kukata mabua, kusaga magunzi, kutoa pumba na kuchakata malighafi mbalimbali kwa ajili ya lishe ya mifugo.

Anasema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano walioupata kutoka COSTECH, ambao uliwasaidia katika hatua za awali za ubunifu pamoja na kuwaunganisha na fursa za uwekezaji.

“Kupitia COSTECH niliweza kupata fursa ya kwenda Finland kukutana na wawekezaji mbalimbali, na kupitia safari hiyo tulifanikiwa kupata mwekezaji aliyewekeza zaidi ya shilingi milioni 500 katika kampuni yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa sasa kampuni hiyo iko katika mpango wa kujenga kiwanda kikubwa jijini Dodoma kitakachokuwa kikizalisha zana ndogo za kilimo kwa ajili ya soko la Tanzania na Afrika Mashariki.

Akizungumzia uwezo wa mashine hizo, Chengula anabainisha kuwa mashine ya kuchakata mazao inaweza kuchakata hadi magunia 25 kwa saa moja na kufanya kazi kwa takribani saa nne mfululizo kwa kutumia lita moja ya mafuta kwa saa.


Anasema teknolojia hiyo siyo tu inarahisisha shughuli za kilimo bali inatoa fursa za ajira kwa vijana, kwani mjasiriamali anayemiliki mashine hiyo anaweza kupata hadi Shilingi 25,000 kwa saa moja baada ya kutoa gharama za mafuta.

CHANGAMOTO 

Hata hivyo, anasema kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa wataalamu wa kuendesha baadhi ya mashine za kisasa, gharama za malighafi pamoja na ushindani kutoka bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi.

Anaiomba serikali kuwepo kwa mazingira rafiki zaidi kwa wazalishaji wa ndani ili kuwawezesha kushindana na wazalishaji wa nje na kuendelea kukuza teknolojia za ndani.

Chengula anafafanua kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na kutumia majukwaa ya kidijitali kutangaza bidhaa zao ili kufikia wakulima wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.


Post a Comment

0 Comments

MASHINE ZA KITANZANIA ZAVUKA MIPAKA, ZAWAFIKIA WAKULIMA NJE YA NCHI