VETA YAHAMASISHA WAHITIMU KUJIUNGA NA UALIMU WA UFUNDI

Na Asha Mwakyonde,DAR ES SALAAM 

CHUO cha Ualimu wa Ufundi Morogoro kimetoa wito kwa wahitimu wa kidato cha sita na vyuo mbalimbali nchini kutumia fursa ya kujiunga na mafunzo ya ualimu wa ufundi yanayotolewa chuoni hapo, ili kusaidia kuziba pengo la walimu wa ufundi linaloongezeka kufuatia maboresho ya mtaala wa elimu nchini.

Akizungumza leo Julai 1,2026 katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), 'Sabasaba' kwenye banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Morogoro, Ramadhani Msidada, amesema Chuo cha Ualimu wa Ufundi Morogoro kinachosimamiwa na VETA kinatoa mafunzo ya ualimu wa ufundi (amali) kuanzia ngazi ya cheti hadi diploma.

Amesema lengo likiwa ni kuandaa walimu wenye umahiri wa kufundisha katika shule za sekondari zenye mkondo wa ufundi, vyuo vya ufundi na taasisi nyingine za mafunzo nchini.

Amesema kuanzishwa kwa shule za sekondari zenye mkondo wa ufundi kufuatia maboresho ya mtaala wa elimu nchini kumeongeza mahitaji ya walimu wa ufundi, hali iliyoifanya chuo hicho kupanua huduma zake za mafunzo ili kukidhi mahitaji hayo.

Aidha, ameeleza kuwa chuo kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu waliopo kazini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ambapo zaidi ya walimu 100 wamewezeshwa kupata ujuzi wa ufundi ili kuboresha uwezo wao wa kufundisha katika shule za sekondari.

Msidada ameongeza kuwa chuo hicho kinaendelea kupokea wanafunzi wapya katika programu za cheti na diploma, huku wanafunzi wanaokidhi vigezo wakipata fursa ya mikopo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, jambo linalorahisisha kugharamia masomo yao.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania wote wenye sifa kujiunga na Chuo cha Ualimu wa Ufundi Morogoro ili kuchangia upatikanaji wa walimu wa ufundi wenye uwezo wa kuimarisha elimu ya ufundi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments

MALEZI BORA NI UWEKEZAJI WA KIZAZI NA MAENDELEO YA TAIFA - NAIBU WAZIRI MAHUNDI