UWEKEZAJI WA TEA WABADILI MAZINGIRA YA SHULE


📍Waongeza ufanisi wa elimu nchini 

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

MABORESHO ya miundombinu ya elimu yanayotekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), yanaendelea kuleta mageuzi makubwa katika shule mbalimbali nchini, huku yakiboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha usalama wa wanafunzi na kuongeza ufaulu wa kitaaluma.

Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa maeneo yanayoshuhudia matokeo hayo kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu inayowanufaisha wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla.

Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW),Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Kiingereza Mohamed Mkoko, anasema s hiyo ni miongoni mwa wanufaika wa miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa TEA.

Mkoko anasema kabla ya utekelezaji wa mradi huo,shule ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa wanafunzi pamoja na mali za shule.

Anaeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya shule, jamii na wadau wa maendeleo, maombi ya ujenzi wa uzio yaliwasilishwa na hatimaye kupatiwa ufadhili, ambapo kwa sasa sehemu kubwa ya uzio imekamilika na hatua za mwisho za ujenzi zinaendelea.

"Tunashukuru kwa msaada tulioupata kupitia TEA na wadau wengine. Mabadiliko yanayoonekana sasa ni makubwa. Ukifika shuleni utaona mazingira yamebadilika kwa kiasi kikubwa na usalama umeongezeka," anasema Mkoko.

Anasema maboresho hayo yameleta matokeo chanya katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji, ambapo wanafunzi sasa wanasoma katika mazingira salama, tulivu na rafiki zaidi.

Kwa mujibu wa Mkoko, uwepo wa uzio umeondoa changamoto ya watu na mifugo kuingia hovyo katika eneo la shule, jambo ambalo hapo awali lilivuruga ratiba za masomo na kuhatarisha usalama wa wanafunzi.

Anabainisha kuwa mazingira bora yaliyopo sasa yameongeza umakini wa wanafunzi darasani huku walimu wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Mbali na ujenzi wa uzio,Mkoko anaongeza kuwa shule mbalimbali katika eneo hilo zimeendelea kunufaika na maboresho ya miundombinu ikiwemo madarasa, mabweni na huduma nyingine muhimu ambazo zimeongeza ubora wa elimu.

"Mazingira ya kujifunzia yameimarika na ari ya wanafunzi pamoja na walimu imeongezeka. Haya ni matokeo ya uwekezaji unaoendelea kufanyika katika sekta ya elimu," anasema.

Aidha,anafafanua kuwa maboresho hayo yameongeza mwamko wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule kutokana na kuongezeka kwa imani juu ya usalama na ubora wa mazingira ya kujifunzia.

Mkoko anasema jamii imeendelea kushuhudia matokeo chanya ya uwekezaji huo na kuahidi kuwa shule itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha miundombinu iliyopo inatunzwa na kuboreshwa zaidi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Meneja wa Miradi kutoka TEA, Mwanafatma Mohamed, anasema mamlaka imeendelea kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo ya elimu nchini ili kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Anasema TEA imeajiri wataalamu wa kada mbalimbali za ujenzi, wakiwemo wahandisi, wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi (Quantity Surveyors), hatua iliyoongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi kuanzia maandalizi ya zabuni, ujenzi hadi ukaguzi wa kazi zinazotekelezwa.

Anaeleza kuwa wataalamu hao hufanya kazi kwa karibu na wataalamu wa Halmashauri mbalimbali ili kuhakikisha miradi yote inakidhi viwango vya ubora na fedha za umma zinatumika kwa ufanisi.

Aidha, anasema TEA inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, wakiwemo UNICEF, katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu.

Anasisitiza kuwa usimamizi huo wa karibu umewezesha miradi ya maendeleo kufikia viwango vinavyotarajiwa na kuendelea kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu nchini.

Post a Comment

0 Comments

UKARABATI WA KITUO CHA KUZALISHA UMEME CHA HALE WAFIKIA ASILIMIA 83 YA UTEKELEZAJI