SELF YAVUKA MALENGO YA FAIDA, YATOA MIKOPO YA BILIONI 43.26


Wajasiriamali 38,545 Wanufaika na Mikopo ya SELF

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

MFUKO wa SELF (SELF Microfinance Fund), umeendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwa wananchi wenye kipato cha chini na wajasiriamali wadogo nchini baada ya kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 43.26 kwa wanufaika 38,545 katika kipindi cha nusu ya mwaka 2025, hatua iliyochochea upatikanaji wa mitaji, kuimarisha shughuli za uzalishaji na kuongeza fursa za ajira katika sekta mbalimbali za uchumi.

Mafanikio hayo yanaonyesha mchango wa mfuko huo katika kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia huduma za kifedha, huku ukiendelea kutekeleza malengo ya Serikali ya kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuimarisha maendeleo ya sekta ya ujasiriamali nchini.

Hayo yamesemwa leo Juni 2, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, wakati akiwasilisha mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2025/26 pamoja na mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/27.

Amesema kuwa kwa mwaka 2025, SELF  ilipanga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 48 ikilinganishwa na shilingi bilioni 45.2 zilizotolewa mwaka 2024.

Aidha, ameeleza kuwa mfuko huo ulilenga kuongeza faida kabla ya kodi hadi shilingi bilioni 1.14 kutoka shilingi bilioni 1.09 za mwaka uliotangulia.

Balozi Omar amesema mfuko huo pia ulipanga kuongeza mtaji wake kutoka shilingi bilioni 58.99 mwaka 2024 hadi kufikia shilingi bilioni 61, kuongeza idadi ya wateja kutoka 55,743 hadi 60,000, pamoja na kuongeza kiwango cha marejesho ya mikopo iliyoko ndani na nje ya mizania ya mfuko.

Amefafanua kuwa hadi Desemba 2025, SELF ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 43.26 kwa wajasiriamali wadogo 38,545, sawa na asilimia 90.13 ya lengo la mwaka.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, sekta zilizonufaika na mikopo hiyo ni pamoja na huduma za fedha zilizopokea shilingi bilioni 22.40, biashara shilingi bilioni 9.43, mikopo binafsi kwa matumizi ya kawaida shilingi bilioni 8.66, kilimo shilingi bilioni 1.90 na ujenzi shilingi bilioni 0.87.

Aidha, ameongeza kuwa SELF ilipata faida ya shilingi bilioni 2.29, sawa na asilimia 200.88 ya lengo lililowekwa, mafanikio yanayoonyesha kuimarika kwa utendaji wa mfuko huo na uwezo wake wa kujiendesha kwa tija.

Waziri huyo amesema katika kipindi hicho, mtaji wa mfuko ulifikia shilingi bilioni 59.93, sawa na asilimia 98.25 ya lengo la kufikia shilingi bilioni 61.0. Vilevile, idadi ya wajasiriamali walionufaika ilifikia 38,545, sawa na asilimia 101 ya lengo lililowekwa.

Akizungumzia marejesho ya mikopo, SELF ilikusanya shilingi bilioni 1.49 kutoka mikopo iliyo nje ya mizania ya mfuko, sawa na asilimia 74.50 ya lengo, huku ikikusanya shilingi bilioni 41.63 kutoka mikopo iliyo ndani ya mizania, sawa na asilimia 95.93 ya lengo.

Amefafanua kuwa mfuko huo ulizalisha mapato ya jumla ya shilingi bilioni 9.71 hadi Desemba 2025, sawa na asilimia 80 ya lengo la mwaka, hatua inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa shughuli zake za kifedha na mchango wake katika kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments

SELF YAVUKA MALENGO YA FAIDA, YATOA MIKOPO YA BILIONI 43.26