📍Dorice abuni ndege ya rimoti kuboresha mafunzo ya wanaanga
Na Asha Mwakyonde, TANGA
MHITIMU wa kozi ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege kutoka
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),Dorice Msafiri, ameibua ubunifu unaolenga kuboresha mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa fani za anga ikiwa ni kutoka nadharia za darasani hadi kwenye ndege inayoweza kuonyesha kwa vitendo namna inavyobadilisha mwelekeo ikiwa angani.
Amebuni ndege inayodhibitiwa kwa kutumia rimoti (remote-controlled aircraft) kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kuelewa kwa vitendo namna mifumo ya udhibiti wa ndege (flight control systems) inavyofanya kazi.
Akizungumza leo Agosti 17,2026 katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu yanayoendelea mkoani hapa amesema mradi huo umeandaliwa mahsusi kuwa nyenzo ya mafunzo kwa wanafunzi wanaosomea Uhandisi wa Anga (Aeronautical Engineering) na Urubani (Piloting), ili waweze kuelewa namna ndege inavyodhibitiwa kabla ya kuruka, ikiwa angani na baada ya kutua.
Kwa mujibu wa Msafiri, mfumo huo unatumia transmitter iliyopo kwenye rimoti na receiver iliyowekwa ndani ya ndege. Anapotoa amri kupitia rimoti, transmitter hutuma mawimbi ambayo hupokelewa na receiver, kisha kupeleka maelekezo kwenye servos zinazodhibiti sehemu mbalimbali za ndege.
Amesema moja ya malengo ya mradi huo ni kuonyesha kwa vitendo namna primary flight controls na secondary flight controls zinavyofanya kazi.
Ameeleza kuwa primary flight controls zinajumuisha ailerons, elevator na rudder, ambazo humsaidia rubani kudhibiti mwelekeo na mwendo wa ndege, huku secondary flight controls zikijumuisha flaps, zinazosaidia katika hatua mbalimbali za uendeshaji wa ndege.
“Mradi huu umetengenezwa kwa ajili ya kuonyesha control surfaces za ndege na baadhi ya vifaa vinavyomsaidia rubani kubadilisha mwelekeo wa ndege akiwa angani,” amesema.
Msafiri ameongeza kuwa tofauti na magari ambayo hubadilisha mwelekeo kwa kutumia usukani, ndege hutumia flight control surfaces kufanya mabadiliko ya mwelekeo inapokuwa angani.
Ameeleza kuwa ndege hiyo ina propellers zinazotoa msukumo unaoiwezesha kusonga mbele, ambapo zinapozunguka husukuma hewa kuelekea nyuma na kuisukuma ndege mbele.
Amesema matumizi ya ndege hiyo kama kifaa cha mafunzo yatawasaidia wanafunzi kuona moja kwa moja namna mifumo mbalimbali ya ndege inavyounganishwa na kufanya kazi, badala ya kutegemea nadharia pekee.
Msafiri amefafanua kuwa kwa kutumia rimoti hiyo, mwanafunzi anaweza kutoa amri na kuona namna control surfaces zinavyosogea, hivyo kuelewa uhusiano kati ya amri inayotolewa, mwendo wa sehemu za ndege na mabadiliko ya mwelekeo.
Msafiri amesema mradi huo unaweza kutumika kuwafundisha wanafunzi namna mifumo ya udhibiti wa ndege inavyofanya kazi katika hatua tofauti za safari, ikiwemo kabla ya kuruka, wakati ndege ikiwa angani na baada ya kutua.
Ameeleza kuwa maarifa hayo ni muhimu kwa wanafunzi wanaojiandaa kuwa wahandisi wa ndege pamoja na marubani, kwa kuwa yanawajengea uelewa wa mifumo inayowezesha ndege kufanya kazi kwa usalama.
Amesema mradi huo pia unalenga kuunganisha maarifa ya darasani na mafunzo ya vitendo, ili wanafunzi waweze kuelewa kwa urahisi zaidi dhana za kiufundi zinazohusiana na mifumo ya udhibiti wa ndege.
Ubunifu huo unaonyesha namna vijana wanaosoma na kuhitimu katika fani za sayansi na teknolojia wanavyoweza kutumia maarifa yao kutengeneza vifaa vya mafunzo vinavyosaidia kuimarisha uelewa wa vitendo na kukuza ubunifu katika sekta ya anga.


0 Comments