Na Asha Mwakyonde,TANGA
NAIBU Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Profesa Razack Lokina amesema wakati
Tanzania ikihitaji kuongeza ajira na matumizi ya teknolojia katika kutatua changamoto za wananchi, vijana na watafiti wa UDOM wameonyesha bunifu zinazolenga kuunganisha maarifa ya kitaaluma na mahitaji halisi ya jamii.
Akizungumza leo Agosti 17,2026 jijini hapa alipotembelea banda la Chuo hicho katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara alisema UDOM kimeshiriki katika maonesho hayo kwa kuonyesha tafiti na bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto za jamii.
Amesema baadhi ya bunifu zilizoonyeshwa zimetengenezwa na walimu na wanafunzi wa chuo hicho, zikiwemo teknolojia zinazoweza kusaidia katika ufuatiliaji wa simu iliyopotea au kuibwa, pamoja na vifaa vya kupima unyevu kwenye mazao.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo inaweza kumsaidia mkulima kubaini hali ya mazao yaliyohifadhiwa kwenye magunia na kufahamu kama yameathirika kwa unyevu au yako katika hali nzuri.
Aidha, amesema UDOM imeonyesha bunifu nyingine zinazohusiana na afya, ikiwemo teknolojia zinazosaidia katika ufuatiliaji wa magonjwa mbalimbali kama magonjwa ya figo na moyo, pamoja na tafiti zinazohusu lishe bora kwa wagonjwa.
Ameongeza kuwa maonesho hayo ni fursa kwa wananchi wa Tanga na maeneo jirani kujifunza kuhusu tafiti na teknolojia zinazozalishwa na chuo hicho, huku akibainisha kuwa baadhi ya bunifu hizo zinaweza kutumika katika tafiti zaidi ndani na nje ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, amesema UDOM imeandaa programu mpya za masomo katika ngazi za uzamivu na uzamili, ikiwemo programu zinazohusiana na uchumi na maendeleo.
Amewahimiza vijana waliomaliza shahada ya kwanza kutumia fursa hiyo kuomba masomo katika programu hizo pindi zitakapotangazwa, huku akiwataka kufuatilia tovuti na mitandao rasmi ya chuo hicho ili kupata taarifa kuhusu programu mpya na masharti ya kujiunga nazo.
Vijana wametakiwa kutumia maonesho ya tafiti na ubunifu kama fursa ya kuonyesha uwezo wao kwa jamii, taasisi za umma na binafsi ili kupata nafasi za kushirikiana, kuajiriwa na kuendeleza bunifu zao.
Prof. Lokina ameeleza kuwa maonesho hayo ni sehemu ya kuwawezesha wadau mbalimbali kutambua bunifu zinazozalishwa na vijana na kuona namna zinavyoweza kutumika kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Ametoa mfano wa bunifu inayosaidia kupima unyevu katika mazao yaliyohifadhiwa kwenye maghala, akisema teknolojia hiyo inaweza kuwasaidia wafanyabiashara, wakulima na wafugaji wanaohifadhi mazao yao katika maghala kubaini mapema kama kiwango cha unyevu kinaweza kuathiri ubora wa mazao.
Amesema teknolojia kama hiyo inaweza kuwa na manufaa katika biashara ya mazao, ikiwemo kuhakikisha bidhaa zinazokusudiwa kusafirishwa au kuuzwa nje ya nchi zinakidhi viwango vinavyohitajika.
Aidha,amefafanua kuwa bunifu zinazozalishwa na vijana zinaweza kuwa chanzo cha ajira endapo zitatumiwa na kuendelezwa na taasisi za umma, sekta binafsi na wafanyabiashara.
“Maonesho haya yanatoa fursa kwa taasisi za umma na binafsi kuona namna zinavyoweza kufanya kazi na vijana wanaobuni teknolojia mbalimbali,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hizo yanaweza kuwasaidia baadhi ya vijana kupata ajira, huku wengine wakipata fursa ya kujiajiri na kuendelea kubuni bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya jamii.
Amehimiza wadau kutembelea maonesho hayo na kujionea bunifu zinazotolewa na vijana, akisema ushirikiano kati ya wabunifu, taasisi na sekta binafsi ni muhimu katika kugeuza ubunifu kuwa fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi.


0 Comments