ELIMU YA MSINGI YAONWA NGUZO YA TANZANIA YA 2050

Na Asha Mwakyonde, TANGA

MHADHIRI kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Dk.Kelvin Swai amesema Tanzania ya mwaka 2050 inaanza kujengwa leo, ndani ya madarasa ambako watoto wanaotarajiwa kuwa wahandisi, wajasiriamali, wakulima, wataalamu na viongozi wa kesho wanapata maarifa na kujenga uwezo.

Pia uwekezaji katika elimu ya msingi inayozingatia ujuzi ni hatua muhimu katika kuiandaa nchi kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, uchumi na mazingira duniani ambapo matarajio ya Tanzania kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 hayawezi kutimia bila kujenga msingi imara wa maarifa, ujuzi na uwezo wa watoto tangu ngazi ya elimu ya msingi.

Akizungumza leo Agosti 17,2026 katika Kongamano la Kitaifa la Elimu, Utafiti, Ujuzi na Ubunifu lililoandaliwa na Wizara ya Elimu Sanyansi na Teknolojia katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara amesema mwaka 2050 haupaswi kuonekana kuwa ni jambo la mbali, kwa kuwa ni miaka 24 tu kutoka sasa, hivyo maandalizi ya kizazi kitakachokuwa mstari wa mbele katika kuijenga Tanzania hiyo yanapaswa kuanza sasa.

Amesema watoto waliopo shuleni leo ndio watakaokuwa sehemu ya utekelezaji wa matarajio ya Taifa mwaka 2050, hivyo aina ya elimu wanayopewa sasa itaamua kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kukabiliana na changamoto na kutumia fursa zitakazojitokeza baadaye.

“Watoto tunaowataka waishi na kufurahia mafanikio ya Dira ya 2050 wapo katika madarasa yetu leo. Wahandisi, wajasiriamali, wakulima na viongozi wa kesho wako shuleni sasa,” amesema.

Dk. Swai amesisitiza kuwa mjadala kuhusu elimu haupaswi kuishia katika kuongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa shuleni au kujenga madarasa na miundombinu, bali unatakiwa kuelekezwa zaidi katika ubora wa ujifunzaji.

Ameongeza kuwa ni muhimu kujiuliza iwapo watoto wanajifunza kwa ufanisi, wanaelewa wanachofundishwa na kama wanaweza kutumia maarifa hayo kutatua changamoto zinazowazunguka katika familia, shule na jamii zao.

Kwa mujibu wa Dk. Swai, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupanua upatikanaji wa elimu tangu uhuru, ikiwemo kuongeza uandikishaji wa wanafunzi, kujenga madarasa na kuboresha miundombinu ambapo hatua inayofuata inapaswa kuwa kuhakikisha elimu inayotolewa inawajengea watoto uwezo wa kufikiri kwa kina, kubuni na kutatua changamoto.

Amesema dunia inabadilika kwa kasi katika teknolojia, uchumi na mazingira, hivyo Tanzania inahitaji vijana wenye uwezo wa kufikiri kimkakati, kuwasiliana, kubuni na kuendana na mabadiliko ili waweze kushindana ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Profesa Ladslaus Mnyone, amesema ni muhimu Tanzania kujenga rasilimali watu yenye uwezo wa kufikiri kwa kina na kimkakati, pamoja na kutumia maarifa na ujuzi kutafuta suluhisho nje ya mazoea ya kawaida.

Amesema mijadala inayofanyika katika maadhimisho hayo inalenga kukusanya maoni yatakayosaidia Serikali kuweka mikakati ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya miaka 50 ijayo.

Prof. Mnyone amesema maazimio yatakayopatikana katika mijadala hiyo yataunganishwa na kuandaliwa katika hati ya kitaalamu (Technical White Paper) ambayo itawasilishwa katika ngazi za Serikali kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

“Hatutarajii makongamano haya yaishie kuwa sherehe au mikusanyiko ya kujadili mambo bila utekelezaji. Ni lazima tutoke na maazimio yanayoonyesha hatua tunazopaswa kuchukua kutokana na yale tutakayojadili,” amesema.

Ameelza kuwa maoni ya wadau wa elimu, elimu ya juu, sekta binafsi, sayansi, teknolojia na ubunifu yatasaidia kuandaa msingi wa utekelezaji wa mipango yenye lengo la kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Maandalizi ya Tanzania ya mwaka 2050 yanahitaji kuanza na mtoto wa leo, kwa kuhakikisha elimu ya msingi haimwandai mwanafunzi kwa ajili ya kufaulu mitihani pekee, bali inamjengea uwezo wa kutumia maarifa, kubuni, kutatua changamoto na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments

BRELA: UBUNIFU USIISHIE KUWA WAZO, YATAKA UGEUZWE MALI