BRELA: UBUNIFU USIISHIE KUWA WAZO, YATAKA UGEUZWE MALI

Na Asha Mwakyonde, TANGA

KATIKA zama ambazo teknolojia inabadilisha maisha kwa kasi, wazo la ubunifu linaweza kuwa zaidi ya suluhisho la changamoto, linaweza kugeuka kuwa mali yenye thamani, chanzo cha ajira na fursa ya kipato kwa mbunifu na kwamba ubunifu usiolindwa unaweza kupoteza thamani na kutumiwa na wengine bila ridhaa ya mbunifu.

Hayo yameelezwa leo Agosti 17,2026 na Afisa Usajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Benedickson Byamanyilwowa, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu yanayoendelea mkoani hapa amesema wabunifu wanapaswa kuhakikisha kazi zao, ikiwemo nembo, michoro, bidhaa mpya na teknolojia mbalimbali zinasajiliwa ili kupata ulinzi wa kisheria na haki ya kipekee ya kuzitumia.

Amesema usajili unampa mbunifu fursa ya kutumia ubunifu wake kibiashara, kuuza haki zake au kuingia makubaliano na taasisi na watu wengine wanaohitaji kutumia au kuendeleza teknolojia hiyo.

“Ubunifu uliosajiliwa unakuwa mali yenye thamani ambayo mbunifu anaweza kuiuza, kuingia makubaliano na mtu au taasisi nyingine kuitumia au kuendeleza teknolojia hiyo na kupata manufaa ya kifedha,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa teknolojia zinazolenga kutatua changamoto za jamii, ikiwemo matumizi ya akili bandia (AI) na vifaa vinavyosaidia watu wenye ulemavu, zina uwezo wa kuwa na thamani kubwa endapo zitalindwa na kusajiliwa ipasavyo.

Ametolea mfano wa miwani maalumu inayoweza kumsaidia mtu mwenye changamoto ya kuona, akisema ubunifu kama huo unaweza kuwa mali yenye thamani na kumwezesha mbunifu kunufaika kiuchumi.

Byamanyilwowa amewahimiza wabunifu, wanafunzi, walimu na wataalamu wa teknolojia kutumia fursa ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu kujifunza taratibu za usajili na ulinzi wa ubunifu ili kuugeuza kuwa fursa ya kiuchumi na suluhisho la changamoto za jamii.


Post a Comment

0 Comments

BRELA: UBUNIFU USIISHIE KUWA WAZO, YATAKA UGEUZWE MALI