Na Jackline Minja – WMJJWM, Arusha
SERIKALI imeendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji wanawake kiuchumi, ikiwemo kuwawezesha kupata mitaji na mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, wakati akifungua Kongamano la Usimamizi wa Biashara na Uchumi lililoandaliwa na Wanawake Laki Moja, jijini Arusha, akisisitiza umuhimu wa wanawake kuwa na ujuzi wa kusimamia biashara zao ili ziweze kukua na kuwa endelevu.
Naibu Waziri Mahundi amewataka wanawake wajasiriamali kuwa na nidhamu na uwajibikaji kwa kutumia fursa zinazopatikana, ambapo amefafanua kwamba, uwezeshaji wa kiuchumi haupaswi kuishia katika upatikanaji wa mitaji pekee, bali unapaswa kuambatana na maarifa ya usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu, mipango ya biashara, masoko na matumizi ya teknolojia.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kunufaika na fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi ,kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji. Kwa mfano, kupitia utaratibu wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, asilimia 4 hutengwa kwa wanawake, ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi,” alisemaNaibu Waziri Mahundi.
Aidha Naibu Waziri Mahundi amewataka wanawake kutumia teknolojia za kidijitali kutangaza bidhaa, kuwasiliana na wateja, kufanya malipo na kutafuta masoko mapya, huku akisisitiza kuwa mwanamke wa Tanzania anapaswa kuwa si mtumiaji wa teknolojia pekee, bali pia mbunifu, mzalishaji na mshiriki katika uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wake, Mlezi na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa Wanawake Laki Moja Tanzania, Tano Mwera, amesema kuanzishwa kwa mtandao huo kuna lengo madhubuti la kuwawezesha wanawake kupata ujuzi na elimu mbalimbali zitakazowasaidia katika shughuli zao za kiuchumi.
Tano amesema mtandao huo unalenga zaidi kuwajengea wanawake uwezo katika masuala ya biashara, kuwaongezea uelewa wa namna ya kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kuwawezesha kujenga uchumi imara ambao utasaidia kulinda na kuimarisha familia zao.
Kongamano hilo la Usimamizi wa Biashara na Uchumi limefanyika jijini Arusha na kuwakutanisha wanawake kutoka maeneo mbalimbali nchini pamoja na wadau wa maendeleo ya biashara na uchumi.






0 Comments