KUTOKA KUHITAJI MSAADA HADI KUWA FUNDI, SAFARI YA ERNEST VETA YAMHAKIKISHIA KUONGEZA ELIMU


Na Asha Mwakyonde, TANGA

ULEMAVU haujawa kikwazo cha ndoto, bali umekuwa daraja la kufungua milango mipya ya elimu, ujuzi na kujitegemea kwa watu wenye mahitaji maalum, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha kutumia vipaji vyao katika kujenga maisha na kuchangia maendeleo ya jamii.

Akizungumza leo Agosti 23, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, alipotembelea banda la VETA, katika wiki ya Wiki ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu, inayoendelea kwenye Viwanja vya michezo shule ya Sekondari Usagara jijini hapa amesema Serikali itaendelea kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kupata mafunzo ya muda mrefu ya ufundi, ikiwamo kugharamia ada, ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kutumia ujuzi wao katika shughuli za uzalishaji.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya ufundi, Kasore amesema watu wenye mahitaji maalum wana uwezo mkubwa wa kujifunza na kufanya kazi mbalimbali endapo watapewa fursa, mafunzo na mazingira rafiki ya kuwaendeleza.

Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia watu hao nafasi za mafunzo na kugharamia ada zao, akiwataka wanaohitaji fursa hiyo kujiandaa na kufuata taratibu zilizowekwa.

“Jipange, Januari uanze masomo pamoja na mwalimu wako. Serikali itafanya utaratibu wa kukupatia ada kama ilivyo kwa wale walioanza mwaka huu,” amesema.

Kwa mujibu wa Kasore, mafunzo hayo hayatalenga kuwajengea uwezo wa kutengeneza vifaa pekee, bali yatawapa ujuzi mpana wa kutumia mashine mbalimbali na kutengeneza vifaa vinavyoweza kuwasaidia watu wengine wenye mahitaji maalum.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa baada ya kukamilisha mafunzo, baadhi yao wanaweza pia kupata fursa ya kuwa wasaidizi wa mafunzo na kutumia ujuzi walioupata kuwafundisha wengine.

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wanapata fursa sawa katika elimu, mafunzo na ajira, huku akiwataka wanufaika kutumia nafasi hizo kwa bidii na kujiamini.

“Usikate tamaa. Kila kitu kinawezekana. Jipange kwa ajili ya mafunzo ili uweze kujifunza vitu vingi zaidi, kujua mashine mbalimbali na hatimaye uweze kuwa mwalimu ili uwafundishe wengine,” amesema.

ULEMAVU SI KIKWAZO CHA MAFANIKIO

Awali, mhitimu wa Kozi ya Useremala kutoka VETA Tanga, Erenest Igobeko, amesema fursa ya kupata mafunzo ya ufundi imekuwa muhimu katika kubadili mtazamo wa jamii kuhusu uwezo wa watu wenye mahitaji maalum.

Amesema watu wenye ulemavu wanahitaji kuaminiwa na kupewa fursa kwa sababu wana uwezo wa kufanya kazi mbalimbali na kujitegemea, badala ya kuonekana kama watu wanaohitaji kusaidiwa maisha yao yote.

“Kama sisi watu wenye mahitaji maalum tulivyoweza kufanikisha mambo mbalimbali, naamini na wewe unaweza kufanikiwa. Jambo la msingi ni kujiamini na kuamini kuwa uwezo tulionao unaweza kutuwezesha kufikia malengo yetu,” amesema.

Igobeko ameongeza kuwa baada ya kupata mafunzo ya ufundi, amekuwa na uwezo wa kufanya kazi ambazo awali baadhi ya watu waliona haziwezi kufanywa na mtu mwenye ulemavu wa kuona.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamebadili hata mtazamo wa familia yake, akitoa mfano wa mama yake ambaye awali alikuwa na mashaka kuhusu uwezo wake wa kufanya baadhi ya kazi.

“Nakumbuka siku moja nilipompelekea mama yangu picha ya kiti nilichokuwa nimetengeneza. Alipoiona, alifurahi sana na kusema, ‘Mwanangu sasa amekuwa fundi.’ Hapo niliona kwamba hata mtazamo wa watu wa karibu unaweza kubadilika wanapoona uwezo wetu kwa vitendo,” amesema.

Amefafanua kuwa endapo ataendelea na mafunzo ya muda mrefu kupitia VETA, anaamini ataongeza zaidi ujuzi wake na kuwa na uwezo wa kuwasaidia vijana wengine wenye mahitaji maalum kupata ujuzi na kujitegemea.

Aidha,amesema anatamani kutumia ujuzi huo kuwa mfano na balozi wa watu wenye mahitaji maalum, kwa kuonyesha kwamba ulemavu si kikwazo cha mtu kufanya mambo makubwa.

Igobeko ameeleza kuwa watu wenye mahitaji maalum wanahitaji kupewa fursa, kuaminiwa na kuwezeshwa huku akisema wakipewa mafunzo na mazingira sahihi, wanaweza kufanya kazi, kujiajiri, kuwasaidia wengine na kuchangia maendeleo ya jamii.

Post a Comment

0 Comments

KUTOKA KUHITAJI MSAADA HADI KUWA FUNDI, SAFARI YA ERNEST VETA YAMHAKIKISHIA KUONGEZA ELIMU