RC BATILDA AZINDUA PROGRAMU YA INNOIP


 📍BRELA,COSTECH washirikiana kuinua ubunifu wa watanzania

Na Asha Mwakyonde, TANGA

UBUNIFU wa Watanzania umepewa msukumo mpya wa kutoka kwenye mawazo na tafiti hadi kuwa mali salama za kiakili, bidhaa na fursa za biashara, baada ya kuzinduliwa kwa Programu ya InnoIP Tanzania inayolenga kulinda miliki bunifu na kuharakisha ubiasharishaji wa ubunifu nchini.

Programu hiyo imezinduliwa leo Agosti 22,2026 jijini Tanga na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, wakati wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, ikiwa ni ushirikiano kati ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kupitia DTBi na Buni Innovation Hub.

Akizindua programu hiyo, Balozi Dk. Burian amesema Tanzania inapaswa kuhakikisha mawazo na teknolojia zinazozalishwa na Watanzania zinalindwa, zinaunganishwa na masoko na kutumika kujenga thamani ya kiuchumi na kijamii.

Mkuu wa Mkoa huyo ameeleza kuwa wabunifu wengi wana suluhisho katika sekta mbalimbali kama kilimo, afya, elimu,viwanda na uchumi wa kidijitali, baadhi hushindwa kufikia soko kutokana na ukosefu wa uelewa kuhusu umiliki, ulinzi wa miliki bunifu na fursa za uwekezaji.

"InnoIP itawasaidia wabunifu kupitia mafunzo, kliniki za miliki bunifu, ushauri elekezi, tathmini za ubunifu, msaada wa usajili na mwongozo wa ubiasharishaji.

Balozi Dk. Batilda ametoa wito kwa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kuhakikisha matokeo ya tafiti yanabadilishwa kuwa bidhaa, huduma na suluhisho badala ya kubaki kwenye makabati.

Aidha, amewataka wawekezaji, taasisi za fedha na sekta binafsi kushirikiana na wabunifu wa Kitanzania kupitia uwekezaji, utoaji wa leseni, uendelezaji wa teknolojia na kuwaunganisha na masoko.

Kwa pamoja, viongozi hao wameeleza kuwa InnoIP ni hatua muhimu ya kuhakikisha wazo la Mtanzania halibaki kuwa wazo, bali linalindwa, linakuzwa na hatimaye kugeuzwa kuwa biashara, ajira na thamani kwa Taifa.

Naye Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu na mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Loy Mhando, amesema programu hiyo imeanzishwa kukabiliana na changamoto zinazowakabili wabunifu, ikiwamo kuweka wazi mawazo mapema, kutokuwa na makubaliano ya umiliki na kuchelewa kushughulikia ulinzi wa miliki bunifu.

Amesema InnoIP itawawezesha wabunifu kutambua aina sahihi ya ulinzi kwa bunifu zao, ikiwamo hataza, alama za biashara, hakimiliki, siri za biashara na mikataba ya usiri.

Mhando ameeleza kuwa programu hiyo itawasaidia wabunifu kupitia hatua za uhamasishaji, mafunzo, uchambuzi wa mahitaji, maandalizi, ulinzi, ubiasharishaji na ufuatiliaji.

Sambamba na InnoIP, imezinduliwa pia Programu ya Fursa Women, inayolenga kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali kutumia teknolojia na ubunifu katika kukuza biashara zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu, amesema InnoIP inalenga kubadili mtazamo kuhusu ubunifu kwa kuhakikisha mawazo ya Watanzania yanalindwa, yanaendelezwa na kufikishwa sokoni.

Amesema miliki bunifu si suala la kisheria pekee, bali ni rasilimali ya kiuchumi inayoweza kuvutia uwekezaji, kuwezesha utoaji wa leseni, uhawilishaji wa teknolojia na ujenzi wa biashara.

“Changamoto yetu sasa si kuwa na mawazo pekee; ni kuhakikisha mawazo hayo yanalindwa, yanaendelezwa na yanafika sokoni,” amesema Dk. Nungu.

Amesema mafanikio ya InnoIP hayatapimwa kwa idadi ya waliohudhuria mafunzo pekee, bali pia kwa ongezeko la bunifu zinazolindwa, teknolojia zinazoingia sokoni, biashara zinazokua, uwekezaji unaovutwa na ajira zinazozalishwa.

Programu hiyo, inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya COSTECH na Airtel Tanzania, itawasaidia wanawake kutumia teknolojia katika kutangaza bidhaa, kuwafikia wateja, kufanya malipo, kutunza kumbukumbu na kuboresha uendeshaji wa biashara.

Kwa mwaka wa kwanza, programu inalenga kuwafikia washiriki zaidi ya 5,000 na kufanya tathmini ya mahitaji ya miliki bunifu kwa wabunifu wasiopungua 120.

Post a Comment

0 Comments

RC BATILDA AZINDUA PROGRAMU YA INNOIP