Na Asha Mwakyonde, TANGA
WAFANYABIASHARA wadogo na wa kati sasa wanaweza kutumia teknolojia kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara zao, kutunza kumbukumbu za mauzo na kujenga historia ya kifedha inayoweza kuwa msaada katika kupata huduma za kifedha.
Suluhisho hilo limebuniwa kupitia mfumo wa kidijitali unaojulikana kama Kogpos.co.tz, ambao unawawezesha wafanyabiashara kurekodi shughuli mbalimbali za biashara na kupata taarifa kulingana na siku, wiki au mwezi.
Akieleza kuhusu mfumo huo,katika wiki ya Wiki ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu, inayoendelea kwenye Viwanja vya michezo shule ya Sekondari Usagara jijini hapa mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesoma Shahada ya Biashara katika Mifumo ya Taarifa (Bachelor of Commerce in Information Systems), Lamway Mogen.
Mwanafunzi huyo amesema mfumo huo unalenga kuwasaidia wafanyabiashara kuwa na kumbukumbu sahihi za shughuli zao badala ya kutegemea taarifa zinazoandikwa kwenye daftari.
Amesema mfanyabiashara anaweza kurekodi shughuli zake mbalimbali na kufuatilia mwenendo wa biashara yake kwa kuangalia taarifa za mauzo na shughuli nyingine kwa vipindi tofauti.
“Mfumo unamsaidia mfanyabiashara kuona biashara yake inavyokua, kufuatilia mwenendo wake na kupata taarifa anazoweza kutumia katika kufanya maamuzi,” amesema.
Mogen ameeleza matumizi ya mfumo huo yanaweza pia kumsaidia mfanyabiashara kujenga credit score, kwa kuwa kumbukumbu za shughuli za biashara zinaweza kutoa picha ya mwenendo na uwezo wa biashara husika.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao wakati mwingine hukabiliwa na changamoto ya kukosa kumbukumbu rasmi za biashara wanapohitaji huduma za kifedha.
Kwa mujibu wa mbunifu huyo, mfumo huo pia unalenga kuwasaidia wafanyabiashara kuendana na mabadiliko ya matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa biashara, huku ukiwapa uwezo wa kuelewa kwa kina hali ya biashara zao.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia yanaweza kuwa nyenzo muhimu kwa wafanyabiashara wadogo, kwa kuwa yanawawezesha kupata taarifa sahihi na za wakati kuhusu biashara zao, jambo linaloweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi, kupanga shughuli na kukuza biashara.

0 Comments