ENABEL YAWEKA NGUVU KUIMARISHA UJUZI NA UBUNIFU WA VIJANA,YAWAHAMASISHA KUTIMIZA NDOTO


Na Asha Mwakyonde, TANGA 

KATIKA wakati Tanzania ikihitaji nguvu kazi yenye ujuzi ili kuchochea ajira, uzalishaji na ubunifu, Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (Enabel) Tanzania limeongeza nguvu katika kuimarisha mafunzo ya ufundi na kuwaunganisha vijana kwenye fursa za ajira na kujiajiri.

Jitihada hizo zimeonekana kupitia ushirikiano wa Enabel na Serikali pamoja na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), katika kuunga mkono mashindano ya ujuzi yanayowapa vijana nafasi ya kuonesha uwezo wao, kujifunza kutoka kwa wenzao na kujiandaa kwa ushindani wa soko la ajira.

Akizungumza kuhusu ushiriki wa Enabel katika mashindano hayo, Afisa Mradi wa Wezesha Binti Kigoma kutoka Enabel Tanzania, Abel Mbilinyi, amesema shirika hilo limeingia makubaliano na NACTVET ya kutoa fedha kwa ajili ya maandalizi ya mashindano, ikiwamo ununuzi wa vifaa, zana na mashine zinazotumiwa na vijana wakati wa mafunzo na ushindani.

Amesema Enabel pia imeleta mtaalamu kutoka Ubelgiji mwenye uzoefu katika mashindano ya ujuzi katika mataifa mbalimbali, ambaye anatoa ushauri kuhusu uendeshaji wa mashindano na namna majaji wanavyotekeleza majukumu yao.

“Tunafurahi kushirikiana na Serikali pamoja na NACTVET kuhakikisha ujenzi wa ujuzi katika nchi hii unaendelea. Tunataka kuondoa dhana kwamba ujuzi wa ufundi ni kwa ajili ya wale waliofeli. Hapana,” amesema.

Mbilinyi ameeleza kuwa mashindano hayo yanaonesha kuwa vijana wana uwezo mkubwa wa ubunifu na wanaweza kutengeneza suluhisho mbalimbali endapo watapatiwa mazingira na fursa zinazofaa.

Amefafanua kuwa idadi ya waliofaidika 2350 huku akisema idadi ya ajira ni 430 na kwamba vijana waliopo kwenye mashindano ni watatu ambapo wawili wametoka VETA Tanga na mmoja kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (FDC),Kasulu.

Ameongeza kuwa changamoto si kwamba vijana hao wameshindwa, bali baadhi yao hawajawahi kupata mazingira yanayowawezesha kukuza vipaji na kufikia ndoto zao.

“Ubunifu kama huu unaonesha kwamba hawa vijana si kwamba wameshindwa, bali hawakuwa wamewezeshwa vizuri kufikia ndoto zao. Hizi ndizo ndoto zao mnazoziona sasa wanazifanyia kazi,” amesema.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Utoaji Elimu ya Ufundi kutoka Enabel Tanzania, Thomas Aikaruwa, ameeleza kuwa mpango wa 'Inclusivity' unaotekelezwa na Enabel umeendelea kushirikiana na vyuo mbalimbali vya ufundi nchini, ikiwamo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),na Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA),kwa lengo la kuongeza uwezo wa vyuo na wanafunzi ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Amesema ushirikiano huo unahusisha vyuo vya VETA Tanga, VETA Mwanza, FETA Kigoma na FETA Mwanza, ambavyo vinatoa mafunzo mbalimbali, yakiwamo yanayohusiana na teknolojia ya uvuvi na viumbe wa majini.

Kwa mujibu wa Aikaruwa, Enabel imejikita katika kuongeza uwezo wa walimu na wanafunzi, kuboresha mitaala pamoja na kuvipatia vyuo vifaa vinavyowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

“Ukimuuliza mwanafunzi au mwalimu wa VETA Tanga au VETA Kigoma Enabel imefanya nini, anaweza kueleza mambo mengi, kwa sababu kuna vitu vingi ambavyo vimefanyika, ikiwamo vifaa vilivyowekwa katika karakana na mafunzo kwa walimu,” amesema.

Amesema baadhi ya walimu wamepelekwa katika mafunzo maalumu ili kuongeza uwezo wao wa kufundisha, huku vifaa vya kisasa vikiwekwa katika karakana za vyuo ili kuongeza ufanisi wa mafunzo kwa vitendo.

Aidha, ameongeza kuwa Enabel imekuwa ikishirikiana na taasisi zinazohusika na elimu ya ufundi katika kuboresha mitaala ili kuhakikisha kozi zinazotolewa zinaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Amesema hatua hiyo imewezesha baadhi ya vijana kupata mafunzo ya muda mfupi na kuingia katika soko la ajira wakiwa na ujuzi unaohitajika.

“Kuna vijana wanaopitia kozi za miezi mitatu pekee kwa sababu mafunzo yameandaliwa vizuri na yanaendana na mahitaji ya soko. Mmoja wa vijana hao alisoma kozi ya miezi mitatu na akafanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika mashindano ya eneo lake, na baadaye kuwa miongoni mwa washiriki wa mashindano ya kitaifa,” amesema.

Aikaruwa amesema katika mashindano ya kitaifa ya ujuzi, wanafunzi wawili kutoka Chuo cha VETA,Tanga wamefanikiwa kufika katika hatua hiyo baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya kikanda.

Amebainisha kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo ya uwekezaji unaofanywa katika kuboresha mazingira ya mafunzo, kuongeza uwezo wa walimu na kuwapatia wanafunzi vifaa vinavyowawezesha kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo unafanyika pia kupitia makubaliano rasmi ya ushirikiano (Memorandum of Understanding) kati ya Enabel na taasisi mbalimbali, ukiwa na lengo la kuviwezesha vyuo kufikia hadhi ya Centre of Occupational Skills Excellence.

Kwa mujibu wa Aikaruwa, lengo ni kujenga vyuo vyenye uwezo wa kutoa mafunzo bora, yanayokidhi viwango vya ushindani na yanayoendana na mahitaji ya waajiri.

Amesema Enabel pia itaendelea kushiriki katika mashindano ya ujuzi kwa kusaidia upatikanaji wa baadhi ya vifaa vinavyotumika katika warsha za mashindano pamoja na kuchangia zawadi za washindi.

Afafanua kuwa ushiriki huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Enabel wa kukuza ujuzi, ubunifu na ushindani miongoni mwa vijana, ili elimu ya ufundi isiishie darasani bali iwe daraja la kuwawezesha vijana kupata ajira, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Mashindano ya ujuzi yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadili mtazamo kuhusu elimu ya ufundi, huku vijana wakipewa nafasi ya kuonesha kuwa ujuzi, ubunifu na teknolojia vinaweza kuwa msingi wa kutengeneza ajira na kutimiza ndoto zao.

Post a Comment

0 Comments

ENABEL YAWEKA NGUVU KUIMARISHA UJUZI NA UBUNIFU WA VIJANA,YAWAHAMASISHA KUTIMIZA NDOTO