CFR YATAKA VIJANA KUTUMIA FURSA ZA DIPLOMASIA YA UCHUMI


Na Asha Mwakyonde, TANGA

WAKATI Tanzania ikielekeza nguvu katika kukuza ubunifu, uwekezaji na biashara, Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk. Salim Ahmed Salim (CFR) kimewataka vijana kutambua na kutumia fursa zinazotokana na Diplomasia ya Uchumi ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 inayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga Afisa Uhusiano Mwandamizi wa CFR, Maryciana Mhagama, amesema Diplomasia ya Uchumi ya Serikali inalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania kiuchumi kwa kutumia fursa zinazotokana na ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa.

Ameeleza kuwa Diplomasia ya Uchumi inalenga maeneo mbalimbali ikiwamo uwekezaji, ukuaji wa biashara, mikutano, utamaduni na utalii, huku akisisitiza umuhimu wa Tanzania kutumia fursa zinazopatikana kupitia maeneo huru ya biashara barani Afrika.

“Pamoja na mambo mengine, Uhusiano wa Kimataifa umeweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi, Uwekezaji, ukuaji wa Biashara, Mikutano, Utamaduni na Utalii,” amesema Mhagama.

Ameongeza kuwa CFR pia inaendelea kutoa mafunzo yanayolenga kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuwa mahiri na wenye weledi kitaaluma, wazalendo na raia wema wenye uwezo wa kutoa mchango kwa Taifa.

Kwa mujibu wa Mhagama, kituo hicho kinatoa mafunzo na kozi mbalimbali katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Menejimenti ya Uhusiano wa Kimataifa, Utawala wa Kimkakati pamoja na Diplomasia ya Uchumi.

Amesema fursa hizo ni muhimu kwa vijana wanaotaka kujenga uwezo katika maeneo yanayohusiana na uhusiano wa kimataifa, biashara na uwekezaji.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu nchini ili bunifu zao zisitumike kama maonesho pekee, bali zigeuke kuwa bidhaa na biashara zitakazochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Prof. Mkenda amesema Serikali tayari imeona mafanikio kupitia mashindano ya ubunifu, ambapo baadhi ya bunifu zimefanikiwa kuingia sokoni na kuwa chanzo cha kipato kwa wabunifu.

Miongoni mwa bunifu hizo ni mashine ya kukamua mafuta ya parachichi, mabegi ya shule yenye sola, vifaa vya kusaidia wanafunzi wenye ulemavu, teknolojia za usindikaji wa chakula cha mifugo pamoja na mita janja za maji.

“Lengo ni kuhakikisha bunifu hazibaki kwenye maonesho pekee, bali zinakuwa bidhaa zinazotumika na kuleta matokeo kwa jamii na uchumi,” amesema.

Waziri Mkenda ameeleza Serikali kwa sasa inafuatilia takribani bunifu 70 zilizo katika hatua mbalimbali za maendeleo, huku ikiendelea kushirikiana na taasisi na sekta binafsi kuzisaidia kufikia hatua ya kibiashara.

Aidha, amesema hadi sasa Halmashauri 90 zimeanzisha Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, huku Serikali ikiwa na mpango wa kuyafikisha katika halmashauri zote nchini.

Post a Comment

0 Comments

CFR YATAKA VIJANA KUTUMIA FURSA ZA DIPLOMASIA YA UCHUMI