Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAKATI sekta ya ujenzi ikiendelea kukabiliwa na changamoto za uimara wa miundombinu na athari za mazingira, watafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamebuni teknolojia mbadala za ujenzi zinazolenga kuongeza uimara wa barabara na majengo huku zikisaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Miongoni mwa teknolojia hizo ni NovaCem, DuraCem na DuraCem One A, ambazo zimebuniwa kupitia tafiti za UDSM na tayari zimeanza kupata matumizi katika soko, ingawa bado zinazalishwa kwa kiwango kidogo.
Akizungumza katika leo Agosti 19 katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Mhadhiri Mwandamizi kutoka UDSM, Dk. Makungu Madirisha, amesema NovaCem ni saruji mbadala inayoweza kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali za ujenzi, zikiwemo matofali na paving.
Amesema DuraCem inaweza kutumika katika ujenzi wa tabaka la chini na la juu la barabara, huku DuraCem One A ikiwa ni kionjo kinachochanganywa na lami katika ujenzi wa barabara.
“DuraCem inatumika sana katika kujenga tabaka la juu na tabaka la chini la barabara. DuraCem One A ni kionjo kinachochanganywa na lami mbalimbali,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk. Madirisha, matumizi ya teknolojia hizo yanaweza kuongeza uimara wa barabara, hususan katika maeneo yenye changamoto ya maji yaliyo karibu na uso wa ardhi ambayo huweza kuchangia kuharibika kwa barabara kwa haraka.
Ameeleza kuwa bidhaa hizo pia zina uwezo wa kustahimili mashambulizi ya chumvi na kuwa na uimara unaohitajika katika matumizi mbalimbali ya ujenzi.
TEKNOLOJIA NYINGINE
Dk. Madirisha amesema UDSM pia imebuni bidhaa nyingine iitwayo Bentox, inayoweza kutumika kuziba nyufa pamoja na baadhi ya shughuli za viwandani, ikiwemo utengenezaji wa vifungashio.
Ametaja pia Flax, ambayo inalenga kusaidia kuchuja biogas kwa kuondoa gesi zisizohitajika, zikiwemo carbon dioxide na hydrogen sulfide, hivyo kuboresha ubora wa biogas.
Amesema tafiti hizo zinaendana na jitihada za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuwa sekta ya ujenzi ni miongoni mwa sekta zinazohusishwa na uzalishaji mkubwa wa hewa ukaa.
“Utafiti huu unaenda sambamba na kutafuta masuluhisho ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pia tunaangalia mnyororo mzima wa uchakataji, kwa sababu tunataka kutumia kwa wingi malighafi zinazopatikana hapa Tanzania,” amesema.
CHANGAMOTO YA UZALISHAJI MKUBWA
Hata hivyo, Dk. Madirisha ameeleza kuwa teknolojia hizo bado ziko katika hatua ya uzalishaji mdogo kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa vinavyoweza kuwezesha uzalishaji kwa kiwango kikubwa.
Ameongeza kuwa miongoni mwa vifaa vinavyohitajika ni mashine ya “flash cascade”, ambayo inapatikana China kwa gharama inayokadiriwa kufikia dola 200,000 za Marekani.
“Tunamini tukipata mashine kama hii itaweza kutusaidia kutoka tulipo na kwenda kwenye uzalishaji mkubwa na hivyo kuweza kukidhi mahitaji ya wateja wanaohitaji bidhaa hizi,” amesema.
Amebainisha kuwa baadhi ya bidhaa hizo tayari zimeanza kutumika sokoni, hasa na watu binafsi, huku baadhi ya taasisi za Serikali zikionesha nia ya kuzitumia.
Mhadhiri Mwandamizi huyo amewataka wadau mbalimbali, wakiwemo Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Wizara ya Nishati, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kushirikiana na watafiti wa UDSM ili kukuza matumizi ya teknolojia hizo.
UBUNIFU WA UDSM WATAMBUKULIWA
Dk. Madirisha amesema ubunifu unaofanywa na UDSM umeendelea kutambuliwa kupitia tuzo mbalimbali, ikiwemo tuzo zilizotolewa katika Wiki ya Utafiti na Ubunifu.
Amesema ubunifu huo uliibuka miongoni mwa ubunifu bora wa mwaka na kupata tuzo ya ubunifu wenye kuleta mabadiliko yenye zawadi ya Sh milioni 10 kutoka Kampuni ya Bahari, huku mshindi wa mwaka akipata Sh milioni tano kutoka Benki ya CRDB.
Aidha, amesema binafsi ametambuliwa kutokana na mchango wake katika utafiti na uchapishaji wa machapisho ya kitaaluma katika majarida makubwa ya kimataifa.
Amesema Mei 18 alipokea tuzo ya utafiti kutoka taasisi inayotambua watafiti nchini kutokana na machapisho yake matatu yaliyotambuliwa kwa ubora na athari yake katika utafiti.
Dk. Madirisha amesisitiza kuwa Serikali na wadau wengine wanapaswa kuendelea kuwaunga mkono watafiti ili teknolojia zinazobuniwa nchini zitoke kwenye hatua ya utafiti na kufikia uzalishaji mkubwa, matumizi ya kibiashara na hatimaye kutoa majibu ya changamoto zinazolikabili Taifa.



0 Comments