TUSUMUKE GROUP YALETA MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA KATIKA UFUGAJI WA KUKU


šŸ“Yaonyesha teknolojia zitakazoongeza tija kwa wafugaji Nane nane Dodoma 

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

KAMPUNI ya Tusumuke Group imewahimiza wafugaji wa kuku nchini kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji ili kuongeza tija, kupunguza gharama za uzalishaji na kudhibiti magonjwa yanayoathiri mifugo, huku ikitumia Maonesho ya 33 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) kutoa elimu na kuonesha vifaa mbalimbali vya kisasa vya ufugaji.

Akizungumza leo Agosti 1,2026 katika maonesho hayo, mwakilishi wa kampuni hiyo, Christopher Dioniz, amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa ya kipekee kutokana na kuzinduliwa kwa Mpango Mkakati wa Taifa wa Miaka 10 wa Ufugaji wa Kuku na Waziri Mkuu, jambo ambalo linaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta hiyo.

Amesema kampuni hiyo imeleta vifaa mbalimbali vya kisasa vinavyowezesha wafugaji kuongeza uzalishaji, ikiwemo mifumo ya maji, mfumo wa ufugaji wa kuku kwa kutumia cages unaotumia nafasi ndogo lakini wenye uwezo wa kufuga idadi kubwa ya kuku kwa wakati mmoja.

Aidha, amsema wamewasilisha mashine maalumu inayojulikana kama Fogo, ambayo hutumika kupunguza joto ndani ya banda pamoja na kufanya usafi na uua vijidudu (fumigation), hatua inayosaidia kuzuia milipuko ya magonjwa kabla ya kuingiza vifaranga wapya.

"Baadhi ya wafugaji hufuga aina tofauti za kuku lakini hawafanyi usafi wa kitaalamu kwenye mabanda baada ya kuondoa kuku wa awali. Hali hiyo huongeza hatari ya magonjwa kwa vifaranga wapya. Ndiyo maana tunatoa elimu na kuleta vifaa vinavyosaidia kudhibiti changamoto hiyo," amesema.

Dioniz ameeleza kuwa kampuni hiyo imeleta mashine za kutotolesha vifaranga zenye uwezo wa kuanzia mayai 30 na kuendelea, zinazotumia umeme, betri na nishati ya jua (solar), huku zikitoa matokeo bora ya utotoleshaji kuliko mashine zisizo na ubora.

Ameongeza kuwa banda la kampuni hiyo pia lina vyakula vya kuku pamoja na wataalamu wanaotoa elimu ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji wanaotembelea maonesho hayo.

Akizungumzia usafirishaji wa kuku, amesema kampuni imeleta vibebeo maalumu vya plastiki vinavyolinda kuku dhidi ya majeraha wakati wa usafirishaji, tofauti na matumizi ya matenga au vifaa vingine visivyo salama vinavyosababisha vifo vya kuku baada ya kufikishwa sokoni.

Amewataka wafugaji, wawekezaji na wadau wa sekta ya mifugo kutembelea banda la Tusumuke Group lililopo ndani ya banda la Wizara ya Mifugo ili kujionea teknolojia hizo na kupata elimu itakayowasaidia kuongeza tija na faida katika shughuli za ufugaji wa kuku.

Post a Comment

0 Comments

VETA SINGIDA YATOA TEKNOLOJIA YA SILAGE KUINUA UZALISHAJI WA MIFUGO